Haya hapa magonjwa hatari ya kurithi

Muktasari:
- Magonjwa ya kurithi yanapita kupitia vinasaba na ni changamoto kubwa kwa afya, ikiwemo pumu, kifafa, shinikizo la damu, seli mundu, na baadhi ya saratani. Haemophilia ni tatizo la damu kutoganda, huku kisukari na saratani nyingine pia zinaweza kurithiwa au kuathiriwa na vinasaba na mazingira.
Dar es Salaam. Magonjwa ya kurithi ni aina ya maradhi yanayohama kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia vinasaba.
Miongoni mwa magonjwa hayo ambayo ni sumbufu ni pamoja na pumu, kifafa, shinikizo la damu, seli mundu na saratani.
Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Rare Disease International (RDI), watu milioni 300 duniani kote huathiriwa na magonjwa mbalimbali ambapo asilimia 72 ni yale ya kurithi huku asilimia 70 ya magonjwa hayo huanzia utotoni.
Aidha, miongoni mwa magonjwa hayo ni kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi kama anavyobainisha Dk John Magesa wa Azania Polyclinic. “Tatizo la kutoka na damu nyingi wakati wa hedhi ni ugonjwa wa kurithi unaofahamika kama haemophilia,” anasema.
Anasema ugonjwa huu mara nyingi unasababishwa na upungufu wa protini mwilini ambapo huleta upungufu wa tishu za kufunga damu unapopata jeraha.
Baadhi ya madhara ya yatokanayo na ugonjwa huu ni pamoja na damu kutoganda pale unapopata jeraha.
“Madhara mengine ni damu kuvujia kwenye ubongo, kukusanyika kwenye viungo vya mikono na miguu, majeraha madogo kuwa makubwa na kusababisha kidonda ndugu,” anaeleza. Dalili nyingine za haemophilia ni pamoja na kukojoa mkojo wenye rangi inayoelekea nyekundu, kuwa na madoti mekundu kwenye ngozi ya mwili na kutokwa damu nyingi hata kwenye majeraha madogo.
Ugonjwa mwingine ni saratani ambayo si kila saratani ni ya kurithi, lakini pia kuna aina kadha wa kadha ambazo zinatambulika kuwa ni saratani inayotokana na historia za kifamilia.
Hata hivyo, saratani hizi zinaweza kusababishwa na sababu nyingine nyingi kama mazingira, mtindo wa maisha na mabadiliko yasiyo ya kurithi, ikiwemo saratani ya matiti na shingo ya kizazi.
Ugonjwa mwingine ni kisukari, japokuwa licha ya kutokea pale mwili unaposhindwa kudhibiti kiwango cha sukari au glukosi katika damu, pia ugonjwa huu unaambukizwa kupitia vinasaba.
Kwa mujibu wa Dk Magesa, kila aina ya kisukari ina uhusiano na aina kadhaa za vinasaba. “Aina ya kwanza ya kisukari ni mwili kushindwa kuzalisha insulini ya kutosha na kusababisha glukosi kushindwa kuingia kwenye seli na kusababisha viwango vya sukari kuwa juu (sukari ya kupanda),” anaeleza.
Anataja aina ya pili ya sukari ni pale viwango vya glukosi kwenye damu vinaposhuka chini ya kiwango cha kawaida (sukari ya kushuka).
Katika takwimu za WHO kwa mwaka 2019, kisukari kilisababisha vifo takribani milioni 1.5, huku nusu ya vifo hivyo vikitokea kabla ya umri wa miaka 70 na hasa kwa wagonjwa wenye sukari ya kushuka.
Pumu
Pumu au athma ni ugonjwa wa mfumo wa upumuaji wenye mchanganyiko wa mambo ya kijeni na mazingira, ugonjwa huu unasababishwa kwa kuwa na njia ya hewa kwenye mapafu.
Aidha, Dk Magesa anasema sababu nyingine ya kuwa na pumu ni pamoja na mzio utokanao na vumbi, nywele za wanyama kama paka, hewa chafu au baridi kali, huku chanzo kikuu kikiwa ni vinasaba.
WHO inakadiria kuwa watu wapatao milioni 262 waligundulika kuwa na ugonjwa huo kwa mwaka 2019 na kusababisha vifo takribani 461,000 kwa mwaka, huku maambukizi kwa vijana na watoto yakiongezeka.
Selimundu
Ugonjwa huu hutokana na mabadiliko ya uzalishaji wa protini na haemoglobini katika seli nyekundu za damu ambayo hubeba oksijeni.
Dk Magesa anasema mabadiliko haya mara nyingi husababisha muundo tofauti wa seli nyekundu za damu kutoka duara mpaka umbo la mundu.
Wataalamu wa afya wanathibitisha kuwa ugonjwa huu hurithishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia vinasaba, ambapo jeni moja yenye kasoro hutoka kwa kila mzazi na huungana na kuleta tofauti.
Muunganiko huo wa jeni mbili zenye kasoro husababisha seli nyekundu za damu kuzalisha haemoglobin S badala ya haemoglobini A.
“Uzalishwaji wa haemoglobini S katika mwili husababisha seli nyekundu za damu kuwa ngumu na kuunda umbo la mundu,” anasema.
Selimundu husababisha vifo 34,409 duniani kote, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikiwa ni 81,100, huku ugonjwa huu ukishikilia nafasi ya 12 kati ya vifo vya watoto duniani kote.
Kifafa
Dk Magesa anasema ugonjwa huu mara nyingi hutokea kwenye mfumo wa neva na husababishwa na mabadiliko ya kimawasiliano katika mfumo wa ubongo, hali hii husababisha mshtuko au kizunguzungu na baadaye kuwa na kifafa cha kudumu. “Wataalamu wa afya wanasema, visababishi vya ugonjwa huu ni pamoja na kugonga kichwa na kupata uvimbe kichwani na matatizo mengine ya kiafya, kama vile sukari, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kurithi kutokana na historia za kifamilia,” anaeleza.
Shinikizo la damu
Mara nyingi aina hii ya ugonjwa hurithi kutokana na historia za kifamilia au vinasaba.
Shinikizo la damu hutokea pale nguvu ya damu inayoelekea kwenye kuta za mishipa ya damu inapokuwa juu kuliko kawaida.
Sababu nyingine ya ugonjwa huu ni pamoja na uzito kupita kiasi, kukosa mazoezi, kunywa pombe kupita kiasi, kula chumvi nyingi na magonjwa mengine chochezi kama kisukari, figo na matatizo mengine ya neva.