Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fursa ya matibabu kwa wenye saratani, moyo, afya ya akili Mbeya

Mganga mfawidhi wa Hosptali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Dk Abdallah Mmbaga (wa kwanza kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa madaktari bingwa bobezi. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Kambi hiyo itahusisha madaktari bingwa bobezi 58 kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili (Milembe).

Mbeya. Kambi ya madaktari bingwa bobezi 58 kupitia programu ya Mama Samia, wanatarajia kuweka kambi ya siku tano katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya.

Kambi hiyo itahusisha matibabu ya kitaalamu ya uchunguzi wa afya ya akili, upasuaji wa kibingwa, moyo, figo, saratani, mifupa na uchunguzi wa kina wa magonjwa ya wanawake.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Dk. Abdallah Mmbaga amesema leo Ijumaa, Mei 2, 2025, wakati akitoa taarifa ya ujio wa kambi hiyo itakayoanza Mei 5 mpaka 9, mwaka huu.

Amesema ujio wa madaktari bingwa bobezi ni jitihada za Serikali kuwasogezea huduma wananchi wenye changamoto ambao walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

"Serikali imekuja na programu ya kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi. Lengo ni kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu," amesema.

Dk Mmbaga amesema mpango huo umeratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa Kanda, inayohusisha mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.

"Tunatarajia kuhudumia zaidi ya wananchi 10,000 kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini, kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)," amesema.

Nyingine ni Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili, Taasisi ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa Kanda.

Dk Mmbaga amesema kambi hiyo imelenga kuhudumia wananchi wote wakiwemo wenye changamoto za magonjwa husika.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Agrey Mwaijande amesema mpango huo umekuja mahususi kuondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

"Magonjwa yaliyopewa kipaumbele ni yale ambayo jamii ilikuwa ikilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu ya kiuchunguzi," amesema.

Aidha, amesisitiza jamii kutumia fursa ya kambi ya siku tano ya madaktari bingwa bobezi ili kuepuka kutumia gharama kubwa kufuata huduma za matibabu.

Mkazi wa Forest jijini Mbeya, Recho Pondo ameishukuru Serikali kwa kufikisha huduma hizo ambazo awali walikuwa wakitumia gharama kusafiri kwenda maeneo mbalimbali nchini.

"Tunashukuru kufikishiwa huduma za kibingwa bobezi. Ombi letu, tunaomba Serikali kupunguza gharama za matibabu ili walengwa wafikiwe na huduma," amesema.