Suluhu yatajwa uhaba madaktari bingwa, wabobezi Zanzibar

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui akizungumza kuhusu Wiki ya Afya Zanzibar 2025, visiwani Zanzibar.
Muktasari:
- Zanzibar ina madaktari bingwa 134 na bingwa bobezi wanane pekee, hivyo hulazimika kutumia Sh400 milioni kila mwezi kutibu wagonjwa kupitia rufaa katika hospitali mbalimbali Tanzania Bara.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya Zanzibar, imetaja mikakati ya kukabiliana na uhaba tiba za kibobezi na madaktari bingwa na bobezi, huku ikikaribisha wawekezaji katika sekta ya afya visiwani humo kuelekea utalii wa matibabu.
Mikakati hiyo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, ununuzi wa vifaa na usomeshaji wa wataalamu wa afya katika tiba za kibingwa na bobezi.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Aprili 11, 2025 na Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alipozungumza na Mwananchi kuhusu Wiki ya Afya Zanzibar inayotarajiwa kufanyika kuanzia Mei 4 mpaka 10 mwaka huu, visiwani humo.
Mazrui amesema katika wiki hiyo itakayokutanisha wadau mbalimbali wa afya Tanzania Bara na Visiwani, licha ya kujadili changamoto hiyo, pia itakua fursa adhimu ya kuimarisha mfumo wa afya, kukuza ubunifu katika sekta ya tiba, na kuhamasisha utalii wa afya Zanzibar.
Amesema Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa na bobezi katika tiba, katikati ya safari ya kuelekea utalii wa matibabu.
"Tunao madaktari bingwa 134 ni wachache ukilinganisha na idadi ya watu, wa tiba bobezi ni saba mpaka nane pekee. Sasa ili kutatua hili tayari serikali imewapeleka masomoni zaidi ya madaktari 700 wanasomeshwa kati ya hao ni bingwa na bobezi.
"Madaktari wa moyo mabingwa hawafiki wanne hapo unaona namna gani tutaweza kuongeza zaidi idadi hiyo, tutajenga hospitali zenye uhitaji kwa usahihi tunajenga miundombinu, tunasomesha wataalamu na tunaweka vifaa.
"Kwa sasa tunawapeleka Muhimbili, JKCI, MOI na Ocean Road kila mwezi wagonjwa 200 na si chini ya milioni 400 kwa mwezi tunatumia. Hivyo tunatarajia tukikamilisha mikakati hii tutaweza kuchukua mabingwa kutoka Bara kuja kushirikiana na mabingwa na bobezi wa Zanzibar ili wapate uzoefu," amesema Mazrui.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji
Katika taarifa yake ya Wiki ya Afya Zanzibar 2025, Mazrui amesema wiki hiyo inahusiana moja kwa moja na vipaumbele vya Serikali vilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, pamoja na Mpango wa Mkakati wa Afya wa Zanzibar III.
Amesema wiki hii muhimu ya afya, wanatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha malengo makuu matano.
Waziri Mazrui ameyataja mambo hayo kuwa ni kuongeza uelewa wa Afya kwa jamii, kupitia kampeni za elimu, kambi za afya, na huduma za uchunguzi wa magonjwa bure na kwamba watahamasisha wananchi kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa.
"Kukuza utalii wa afya. Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha utalii wa afya na wellness tourism. Hili litaongeza mapato ya nchi na kutoa ajira kwa vijana wetu.
"Tatu kuboresha ubunifu na teknolojia katika sekta ya afya. Kongamano la siku saba litawapa wadau fursa ya kujadili matumizi ya telemedicine, mifumo ya kidijitali ya afya, na mbinu nyingine za kisasa katika utoaji wa huduma za afya."
Pia amesema watahamasisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), "Tutatumia jukwaa hili kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya, kujenga miundombinu bora ya hospitali, na kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa."
Mazrui ametaja kuimarisha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa afya. Serikali inatambua changamoto wanazokumbana nazo wahudumu wa afya na ndiyo sababu Zanzibar Afya Week 2025 itaweka mkazo kwenye afya ya akili na ustawi wa wafanyakazi wa sekta ya afya.
Mazuri amesema kwa mwaka huu, Zanzibar Afya Week 2025 itafanyika Unguja na Pemba. Shughuli zitaanzia Pemba kwa wiki mbili za matukio makuu matatu, ikiwemo matembezi ya afya, kliniki ya afya ya siku mbili na kongamano la fursa za sekta ya afya.
Amesema Unguja, shughuli zitadumu kwa siku saba kuanzia Mei 4 hadi 10, ambapo kila siku itakuwa na mada maalum na mijadala kuhusu uboreshaji wa sekta ya afya Zanzibar.
Zaidi ya hayo, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa na huduma za afya, upimaji wa bure wa magonjwa katika eneo la tukio Nyamanzi, Unguja, kampeni za uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii kuelekea kilele cha wiki hii.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema wiki hiyo inaakisi dhamira ya Serikali zote mbili na Serikali ya Zanzibar kuimarisha sekta ya afya.
"Tukio hili linalenga kuhamasisha sekta ya afya, taasisi za elimu kwa ujumla na kutoa nafasi ya kushirikiana kupitia malengo mahususi matano ikiwemo
kuongeza uelewa wa afya kwa jamii kupitia elimu kinga na upimaji, kukuza utalii wa tiba kuongeza mapato kwa vijana," amesema Mngereza.
Amesema kongamano hilo pia limelenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kuonyesha ubunifu katika sekta ya afya hatua nyingi zilizofanyika katika matumizi ya mitandao katika kufanya kazi na matibabu yake," amesema.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema mpango huo unakwenda kutoa taswira na majibu katika kutatua changamoto za afya na kuleta tija katika huduma za afya pande zote mbili.