Prime
‘Kaunga’ mabaki ya kuku yenye ladha, lakini hatari kiafya

Muktasari:
- Wataalamu wa afya na lishe washauri kuwe na udhibiti na usimamizi wa biashara ya vyakula.
Dar es Salaam. Mabaki ya viungo vilivyotumika kukaanga kuku na vipande vidogo vya kitoweo hicho maarufu ‘kaunga’ yamegeuka lulu kwa baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, hususani wa kipato cha chini.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya afya wanasema mabaki haya yanayoenguliwa kutoka kwenye mafuta yaliyokaanga kuku ni hatari, yakitajwa kuwa chanzo cha magonjwa yakiwamo ya moyo.
Hatari hiyo inatokana na mafuta yanayotumika kukaanga kuku hao kutumika mara kadhaa na wakati mwingine hadi rangi kubadilika na kuwa mazito kabla ya kubadilishwa.
Katika maeneo ya Buguruni, Tandale na Temeke, biashara ya kaunga hufanyika, mabaki haya yakiuzwa kati ya Sh200 na Sh500 kwa fungu, huku wafanyabiashara wengine wengine wakiyatoa bure kwa wahitaji.

Mfanyabiashara ya kuku wa kukaanga eneo la Buguruni, Zuhura Khamis akizungumza na Mwananchi amesema kwa miezi sita sasa amekuwa akiuza na kugawa mabaki hayo kwa wahitaji, wakubwa kwa wadogo.
“Unakuta mtu hana hela ya kununua kipande cha kuku cha Sh2,000 lakini kaunga ananunua. Biashara inanisaidia hata kama faida ni ndogo, maana hakuna anayekosa kaunga,” amesema Zuhura.
Kwa mujibu wa Zuhura, baada ya kukaanga kuku kadhaa chini ya mafuta hubaki vipande vya ngozi, nyama na viungo kama vile tangawizi na ngano iliyopakwa juu ya kuku kabla ya kukaanga ambavyo ni lazima aviondoe ili kuendelea na kazi.
Kwa upande wake, Baraka Mshika anayekaanga kuku eneo la Mbagala Rangi Tatu anasema awali mabaki hayo alikuwa akiwapa watoto wa shule ya msingi.

Hata hivyo, anasema walikatazwa na wazazi wao, hivyo kwa sasa wateja ni watu wazima.
"Watoto walikuwa wanakuja kuomba nikawa nawapa, baadhi walikwenda nayo nyumbani kwao, ndipo wazazi wakaja wakanizuia nisiwape," anasema.
Anasema watu wazima huweka oda ili awawekee kaunga, ambayo huhuyapitia wanaporudi kutoka kwenye majukumu yao jioni.
Erasto Amos, anayekaanga kuku eneo la Riverside, Ubungo anasema mabaki hayo huyotoa bure kwa wenye kuhitaji.
"Wanakuja kuchukua, nafikiri wanakwenda kula kwa ugali maana wanaokuja wengi ni watu wa makamo na wazee. Huwa wakitaka niwachanganyie na pilipili, hata wanafunzi pia wanakuja kuomba," anasema.
Kwa mtazamo wake, ugumu wa maisha husababisha baadhi ya watu kushindwa kununua kipande cha kuku.
Walaji wataja ladha
Mkazi wa Temeke, Rashid Mbonde mwenye familia ya watoto watatu anasema huvutwa na ladha ya kaunga.
“Sina uwezo wa kula kuku kila siku, lakini kaunga inanitosha. Inakuwa na harufu nzuri na ukiipasha vizuri ni kama nyama tu,” amesema Mbonde.
Muna Ally, mkazi wa Ubungo anasema hula mabaki hayo kama kiburudisho kutokana na ladha yake.
"Siwezi kupitisha siku bila kula mabaki haya, ni matamu hata ukiwa na ugali au mihogo inatosha kabisa. Ladha huwa nzuri zaidi ukikuta hayajaungua sana," anasema.

Mwanafunzi wa shule ya msingi (jina limehifadhiwa) anasema ni kawaida yake kwenda kuomba mabaki hayo kwa wauza kuku ambao humpa bure.
“Yupo muuza kuku anagawa bure kwa wenye kuhitaji, kwa hiyo wanafunzi tukitoka shule tunakwenda kuchukua, tunakuwa wengi maana ni matamu,” anasema.
Hatari kiafya
Wataalamu wa afya wanasema ulaji wa mabaki hayo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa yakiwamo ya moyo, kutokana na namna yanavyoandaliwa na kutunzwa.
Mtalaamu wa chakula na lishe, mkazi wa jijini Dar es Salaam, Fatma Zahran amesema ni hatari kutumia chakula ambacho kimepikwa kwenye mafuta zaidi ya mara moja.
“Mafuta yanapotumika kukaanga mara kwa mara huzalisha kemikali kama polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs) na acrylamide ambazo ni hatari kwa mwili wa binadamu. Kaunga ni mabaki yaliyokaangwa kupita kiasi na ni rahisi kuambukizwa bakteria kutokana na kuhifadhiwa vibaya,” anasema.
Kemikali hizo zinaelezwa kwamba zinaweza kusababisha kansa na kuathiri mfumo wa upumuaji.
Mtaalamu huyo anasema ulaji wa vyakula vilivyokaangwa kwenye mafuta yaliyotumika mara nyingi huongeza hatari ya magonjwa ya ini, saratani na matatizo ya mfumo wa chakula.
Dk Neema Kalala, mtaalamu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amesema matumizi ya mafuta yaliyotumika mara kwa mara ni kichocheo kikuu cha ongezeko la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
“Watu wengi hawajui mafuta yakishatumika zaidi ya mara moja huanza kuharibika kwa kiwango cha kemikali. Yanaweza kuzalisha sumu mwilini na matokeo yake ni matatizo ya afya ya muda mrefu kama vile shinikizo la damu, saratani hata kiharusi,” amesema.
Dk Kalala amesema wananchi wengi huathirika bila kujua chanzo hasa cha matatizo ya kiafya wanayopata.
“Chakula kinaonekana kitamu, lakini madhara yake ni makubwa. Tunashauri watu watumie mafuta safi kila wanapopika, hasa kwa vyakula vinavyokaangwa,” amesema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Tatizo Waane amesema mafuta hayo ni hatari kwa kuwa mtu mmoja anatakiwa kutumia mafuta ujazo wa nusu dole gumba (kijiko kidogo cha chai) kwa siku na asizidishe.
Amesema mafuta mengi yanapoliwa katika chakula, uwezekano wa kupata shinikizo la damu ni mkubwa.
“Usile chukuchuku, umuhimu wa mafuta mwilini upo ila yaliwe kiasi. Kuna vitamini aina nne A, B, C na E zinaingia mwilini iwapo chakula kina mafuta lakini yasiwe mengi,” amesema.
Mamlaka zichukue hatua
Wachambuzi wa afya ya jamii na mazingira wametaka halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam kufanya ukaguzi wa kina kwa shughuli zote za kuuza chakula mitaani ili kudhibiti usalama wa afya kwa wananchi.
Mshauri wa afya ya jamii na mazingira jijini Dar es Salaam, Neema Mwakalinga amesema kuna haja kwa serikali kutoa elimu ya chakula kwa wafanyabiashara ili kuondoa hali inayojitokeza.
“Tunaelewa ugumu wa maisha, lakini ni muhimu kwa mamlaka kuweka viwango na kuwapa elimu wajasiriamali wa chakula mitaani. Hili suala la kaunga linaweza kuwa janga la kimya-kimya kiafya,” amesema.
Hadi sasa, hakuna sheria au kanuni inayodhibiti uuzaji wa mabaki kama kaunga, jambo linalofanya shughuli hiyo kufanyika bila usimamizi rasmi.
Mtaalamu wa afya ya umma, Dk Ali Mzige amesema chakula kinapaswa kuliwa kama kilivyo, lakini kinapokaangwa sana kwa mafuta ya kurudia kinageuka kuwa na athari kwa mtumiaji.
Amesema mnyama kama kuku hasa wa kisasa tayari amekula vyakula na kukua kwa muda mchache, akipikwa kwa kutumia mafuta yenye joto kali sana na kutumia nishati nyingi, huiva kwa joto kubwa hiv yo kuwa na athari.
“Kuna uwezekano wa kukupa saratani, kama hakulishwa vizuri kwa ubora unapata nyama au vyakula visivyofaa. Mabaki yamepikwa kwa muda mrefu yakiingia mwilini yanaleta athari. Si chakula safi na salama,” amesema