Jafo: Utekelezaji viwanda 100 kila mkoa umefika nusu ya lengo kitaifa

Muktasari:
- Mwaka mmoja sasa tangu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alipowataka wakuu wa mikoa kuhakikisha wanajenga viwanda 100 kwenye maeneo yao. Kwa tathmini iliyofanywa miezi sita baada ya agizo hilo, waziri anasema utekelezaji ulikuwa umefika takriban nusu ya malengo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema sera ya ujenzi wa viwanda inatekelezwa kwa vitendo na mpaka sasa kuna jumla ya viwanda 1,280 nchini.
Anasema ujenzi wa viwanda hivyo una-tokana na ushirikiano wake na wakuu wa mikoa ambao aliwataka kuhakikisha wanajenga viwanda 100 kila mmoja ndani ya mwaka mmoja kuanzia mwishoni mwa mwaka jana.
“Kwa tathmini ya awali iliyofanyika Aprili 20, imenifurahisha kwani tumebaini kuna jumla ya viwanda 1,280 sawa na asil-imia 49.2 ya viwanda vinavyotakiwa nchi-ni,” anasema Jafo.
Lengo la Serikali, anasema ni kuhak-ikisha mpaka Desemba mwaka huu kila mkoa uwe umejenga viwanda vidogo na vya kati visivyopungua 100 hivyo kufikisha viwanda 2,600 nchi nzima.
Waziri Jafo anasema Serikali imekusu-dia kuwa nchi ya kipato cha kati kupitia viwanda hivyo wakuu wa mkoa wanataki-wa kuhakikisha wanahamasisha viwanda vidogo na kati kwa kuwashirikisha vion-gozi na wananchi katika maeneo yao ya utawala.
Katika kusimamia utekelezaji wa agizo hilo, anasema ofisi yake itaweka utaratibu maalum wa kupima utendaji wa kila mkuu wa mkoa kwa kuangalia ushiriki wake wa kuwajengea hamasa viongozi wa chini wakiwemo wakuu wa wilaya na wananchi.
“Serikali itatoa vyeti kwa mikoa itakayofanya vizuri katika ujenzi wa viwanda. Hii inalenga kutoa motisha kwa mikoa iliyobaki kujifunza na kubaini mbinu mbadala za kuibua viwanda ili kuwakomboa wananchi kiuchumi,” anasema Jafo.
Waziri huyo anasema kufanikisha ujenzi wa viwanda nchini, Serikali inaweka kipaumbele kuhakikisha upatikanaji wa malighafi hasa za kilimo jambo litakalofanikiwa kwa wakuu wa mikoa wanawatumia vyema maofisa ugani kutekeleza majukumu yao.
Amewataka wakuu wa mikoa nchini kusimamia vyema ukusanyaji mapato ya ndani na kuwawezesha wananchi kupata mikopo ili kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa viwanda. Ili wakopesheke, waziri huyo ameagiza: “Wakuu wa mikoa kupitia kwa maofisa maendeleo ya jamii wawahamasishe wananchi kujiunga katika vikundi hivyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi.”
Wasomi wakumbusha
Wasomi nchini wanaamini Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na mtazamo mpana wa kuanzisha viwanda ili kujenga Taifa imara linalojitegemea kiuchumi.
Wakati wa utawala wake, wanasema viwanda alivyoanzisha vilikuwa vya nguo, kubangua korosho, kuchambua pamba na zana za kilimo. Viwanda hivyo, wanasema vilikuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania masikini wanaojishughulisha na kilimo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila anasema ni bahati mbaya mafanikio yaliyofikiwa katika ujenzi wa viwanda hayakudumu kwa muda mrefu. “Viwanda vingi vilivyoanzishwa vilikufa. Pamoja na mambo mengine sababu kubwa ya kufa kwa viwanda hivyo ni uongozi na uendeshaji mbaya, hujuma na ukosefu wa uadilifu na uzalendo,’’ anasema.
Viwanda vya enzi za Mwalimu vilijengwa ili kuimarisha uchumi kwa kuchakata malighafi za wakulima na kutengeneza bidhaa kabla ya kuuzwa katika soko la ndani na nje ya nchi. Mwalimu aliamini ili Tanzania iendelea, ni lazima pawepo viwanda vya kutosha.
Katibu mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustine Kamuzora anasema dhana ya kujitegemea kuanzia ngazi mtu binafsi, familia hadi Taifa ni kongwe kama ilivyo historia ya mwanadamu.
Anasema wanazuoni mbalimbali wamefafanua umuhimu wa kujitegemea kiuchumu kwa kutambua unyonge ndio chanzo cha kushindwa kujitegemea na kujiamria mambo binafsi.
“Mwaka 1962 Mwalimu aliwaasa Watanganyika kuwa hawawezi kuwa na uhuru wa kweli ikiwa Taifa linajiendesha kwa kutegemea zawadi,’’ anakumbusha.
Tangu mwanzo wa harakati zake za ukombozi hadi mwisho wa maisha yake, anasema Mwalimu Nyerere alipambana kuhakikisha Watanzania na wanyonge wengine duniani wanajitegemea kiuchumi.
Mhadhiri na mkuu wa idara ya stadi za uchumi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Binto Mawazo anasema mataifa mengi duniani yamejikita kukuza uchumi wa viwanda kwa muda mrefu.
Anasema wakati wadau wa maendeleo ya uchumi wakipambana kuukuza kwa ufanisi zaidi, elimu ya kujitegemea inaonekana kuwa na mchango wa kuwaridhisha wadau wengi yakiwamo mataifa yaliyoendelea.
“Tanzania iliitumia nadharia Mwalimu alipolitangaza Azimio la Arusha na kubainisha misingi ya siasa ya ujamaa ambayo chimbuko lake ni elimu ya kujitegemea,” anasema Mawazo.
Hata hivyo, anasema wakati nchi nyingi duniani zilifanikiwa katika matumizi ya nadharia hiyo, Tanzania haikufanya vizuri kwani viwanda vilivyoanzishwa baada ya uhuru hadi mwishoni mwa miaka ya 70, havikuwa na tija endelevu.
Wakati nadharia hii ikisaidia kukuza ufanisi wa maendeleo ya uchumi katika nchi nyingi hasa za Bara la Asia na baadhi ya za Afrika, Watanzania wameendelea kutafuta suluhisho la changamoto zilizosababisha kushindwa kuendeleza viwanda viliovyoanzishwa kwa gharama kubwa.
“Kuna udhaifu mkubwa kuziishi na falsafa za Mwalimu Nyerere juu ya Taifa kujitegemea na maendeleo ya viwanda Tanzania. Tumekuwa nyuma katika kuielimisha jamii kuitumia nadharia ya ujasiriamali kama msingi wa maendeleo ya uchumi,” anasema Mawazo.
Kutokana na changamoto hiyo, anasema wataalamu wengi wanashindwa kujikita katika maeneo yao ya ubobezi ili waweze kutoa mchango ulio na tija hivyo kukosa ufanisi utakaochangia kukuza uchumi.
Mwenendo huu, endapo hautarekebishwa haraka iwezekanavyo, anasema unaashiria uwezekano mkubwa wa kushindwa kufikia uchumi wa kati kwa misingi ya kuchochea maendeleo kwa kutumia nadharia ya maendeleo ya viwanda mpaka ifikapo 2025.
Makamu mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Dk Charles Kitima anasema maendeleo ya viwanda ni lazima ili raia wajipatie mahitaji muhimu kwa gharama nafuu bila kuhitaji kuagiza kutoka nje ya nchi.
Vilevile, anasema bidhaa za viwandani huwaunganisha raia na nchi nyingine kibiashara. Muunganiko na ubadilishanaji wa bidhaa hutegemea ujuzi na teknolojia ya nchi inayozalisha bidhaa husika. “Tutahitaji utashi wa kisiasa na kufanya uamuzi sahihi wa viwanda vya kuanza navyo, kwa teknolojia ipi na wawekezaji gani…ni lazima tubainishe masoko tunayotaka kuyahudumia,” anasema Dk Kitima.
Katika umakini huo, anakumbusha kuwa elimu ni chombo cha lazima katika kuleta mapinduzi na mabadiliko endelevu ya mfumo wa uchumi utakaowagusa wananchi wengi.
Anasema uchumi wa viwanda unahitaji kujenga namna mpya ya watu kufikiri na kuishi na kwamba haya ni mapinduzi ya kiutamaduni yanayomhusu kila raia.
“Kuwaingiza Watanzania katika uchumi wa viwanda ni lazima kutumia mfumo wa elimu rasmi na endelevu kwa watu wazima,” anasisitiza.
Amesema maswali haya yataweza kujibiwa kwa njia ya elimu na mijadala ya kitaaluma ili kuwezesha kuundwa sera na mipango madhubuti ya Tanzania ya viwanda yenye mvuto kimataifa.
“Kwa mantiki hii mfumo wa elimu Tanzania ndio utakaojibu uwezekano wa viwanda kukuza uchumi na kuifanya nchi kuwa moja ya nchi zenye viwanda kwa dhana ya kisayansi,” anasema.
Mkurugenzi mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema Serikali inatakiwa kutoa tafsiri ya viwanda ambavyo inavijenga ili kuliweka wazi suala hilo na kuwahasisha wananchi wakiwa na maana moja ya kinachotarajiwa badala ya upotoshaji kwamba hata ukiwa na mashine nne za kukamua juisi basi ni kiwanda.
“Tunatakiwa tuwe na viwanda ambavyo vinaweza kutoa ajira kwa wananchi hata ukipita nje ya kiwanda hicho unakuta kuna malori ya bidhaa yameegeshwa unajua kweli hapa kuna kiwanda,” anasema Dk Kijo-Bisimba.
Hata hivyo, anasema Serikali inapaswa kupongezwa kwa jitihada zake za kuhamasisha ujenzi wa viwanda lakini ieleze aina ya viwanda ambavyo inavijenga ili wananchi wanufaike kwa ajira.