Hizi ndizo faida za vyama vya ushirika kwa wakulima

Muktasari:
- Mifumo hii ni kama vile; Kangomba, Kibubu, Kadumula, Independent farmers, rumbesa, butula, chomachoma na mingineyo.
Kuna kila sababu ya kuimarisha mazao makuu ya biashara tukianza na mazao makuu ya kimkakati kupitia mfumo wa vyama vya ushirika sanjari na kuondoa mifumo holela ya ununuzi.
Mifumo hii ni kama vile; Kangomba, Kibubu, Kadumula, Independent farmers, rumbesa, butula, chomachoma na mingineyo.
Mifumo holela ya ununuzi imekuwa ikitumika na wafanyabiashara wanaonunua mazao kuwanyanyasa wakulima, kwa kuwalipa malipo kidogo wakati wa mauzo na kuwafanya wasinufaike na mazao yao na hatimaye baadhi yao kukata tamaa na kuacha kulima mazao hayo.
Manufaa ya Ushirika kwa nchi kama Tanzania yako dhahiri. Ushirika ni njia pekee ambayo inawaweka wananchi pamoja na kufanya kazi kwa umoja kama jamii moja kutokana na misingi iliyowekwa na waasisi wetu na maadili yake.
Ushirika unajenga nidhamu ya utu, umoja, ushirikiano na upendo. Kihistoria, Ushirika umetoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Hata wasomi wengi wa mwanzo wa nchi hii walisoma kutokana na jitihada za Ushirika.
Ushirika pia huwezesha kupunguza gharama za uzalishaji pale wakulima wanaponunua pembejeo kwa pamoja. Kupitia ushirika, wanaushirika wanajenga nguvu ya pamoja katika kujadili bei ya mazao yao.
Ushirika pia hurahisisha upatikanaji wa takwimu ikiwa ni pamoja na Serikali kupata kodi au ushuru sahihi ikiwa sekta hii itapewa kipaumbele katika ngazi zote.
Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dk Titus Kamani anawataka maofisa ushirika wawe wabunifu na waondokane na utendaji wa mazoea, ili wawasaidie wananchi kwa sababu ushirika ni silaha ya wanyonge na adui wa matajiri wanaowanyonya wakulima.
“Wananchi wanautaka sana ushirika kwa sababu wamechoka kuibiwa, wamepigika sana na bei za soko huria. Wana matumaini na ushirika mpya kwa sababu hakuna mkulima anayekataa malipo ya awamu ya pili,” anasema.
Ili kuwa na vyama vya ushirika vyenye nguvu kiuchumi na vyenye manufaa kwa wanachama kama ilivyokuwa katika miaka ya 1960 na 1970, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Tito Haule anawahimiza viongozi wa vyama vya ushirika kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kujituma ili kuwainua wakulima na wanaushirika kwa jumla.
Aprili, 2018 akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 pamoja na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha vyama vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya kimkakati ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Aidha, alisema Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa kuhamasisha matumizi ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo mazao hayo yatazalishwa na kukusanywa kupitia katika mfumo wa uendeshwaji wa vyama vya Ushirika ikiwa ni pamoja na kuuzwa kwa njia ya minada chini ya usimamizi wa wadau husika.
Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao hayo matano ya biashara kwa lengo la kuondoa mifumo holela ya ununuzi iliyokuwa ikimnyonya mkulima sanjari na kuongeza mapato ya wakulima. Uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya kibiashara, unatokana na ukweli kuwa kwa kipindi kirefu, uzalishaji umekuwa ukishuka kutokana na kuwepo kwa changamoto kadhaa.
Kwa mfano; katika msimu wa 2015/2016 uzalishaji wa zao la pamba ulishuka kutoka tani 456,814 hadi tani 282,809 msimu wa 2013/2014.
Kwa upande wa zao la tumbaku, uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624msimu wa 2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 msimu wa 2015/2016.
Waziri Mkuu akizungumza Mei 19 na warajis wasaidizi wa vyama vya Ushirika wa mikoa 25 na maofisa Ushirika wa halmashauri za wilaya 140 zinazolima mazao makuu ya biashara; aliwataka vingozii wa ushirika kusimamia ipasavyo mifumo ya masoko ili kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa.
Waziri Mkuu amewahimiza maofisa ushirika kutekeleza maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano juu ya kutumia mfumo wa ushirika na minada kununua mazao.
“Sasa hivi pamba imeanza kuuzwa katika baadhi ya maeneo, na zao linalofuata ni kahawa. Lazima ununuzi ufuate mfumo wa ushirika. Nataka mkasimamie suala hili kwa umakini kabisa. Ninawasihi msikubali kuwe na uonevu, dhuluma na wizi kwa wakulima wetu,” anasisitiza.
Katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, ni wazi kuwa, kuwepo kwa vyama vya ushirika imara, vyenye nguvu na endelevu hauepukiki. Hii inatokana na ukweli kuwa, baadhi ya viwanda vinavyotoa huduma vimejengwa kupitia mfumo wa vyama vya ushirika, Mfano ni viwanda vya kutoa huduma ya kukoboa, kubangua, kusindika na kuchakata mazao mbalimbali.
Viwanda vilivyojengwa na vyama vya ushirika ni pamoja na Kiwanda cha maziwa cha Tanga kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Tanga (TDCU Ltd.), Nronga Women Diary Cooperative Society kilichopo mkoani Kilimanjaro pamoja na Kiwanda cha TANICA kinachomilikiwa na vyama vikuu vya KCU Ltd na KDCU Ltd vyote vya mkoani Kagera.
Hii ni mifano mizuri ya manufaa ya Ushirika nchini, kwani vimesaidia kuongeza ajira kwenye maeneo husika na kuongeza thamani ya mazao.
Katika iaka ya awali ya uhuru wetu, Ushirika ulitoa mchango mkubwa kwenye siasa za nchi yetu kwa kutoa wanasiasa mahiri, wazalendo na waliokuwa wanaguswa na matatizo ya wananchi wao.
Watu kama marehemu Sir George Kahama, ni mfano mmoja tu wa Watanzania waliopata elimu yao kwa nguvu za Ushirika. Ushirika wa kahawa uligharamia masomo yake hadi chuo kikuu huko Uingereza.