Zungu awa Spika wa nane akiahidi kutenda haki kwa makundi yote
Muktasari:
- Ameshika nafasi hiyo baada ya kushinda katika kura za maoni kwa wabunge wa CCM na kisha kushindanishwa kwa kura za pamoja na vyama vingine.
Dodoma. Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu amechaguliwa kuwa Spika wa nane wa Bunge la Tanzania huku akitoa ahadi ya kutenda haki kwa kila mbunge.
Zungu ametangazwa leo Jumanne Novemba 11, 2025 baada ya kupata kura 378 kati ya kura 383 na kuwashinda wagombea wengine wanne kutoka vyama vya siasa.
Wagombea wengine na kura zao walikuwa ni Veronika Tyeah (NLD), Chrisant Ndege (DP) na Amir Yango (ADC) ambao kila mmoja hawakupata kura huku Anitha Mgaya (NLD) na Ndonge Said wa AAFP ambao kila mmoja alipata kura moja.
Katika uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Katibu wa Bunge, Baraka Leorad chini ya Uenyekiti wa Mbunge mteule wa Isiman (CCM), William Lukuvi ambaye kwa mujibu wa Kanuni ndiye mbunge aliyehudumu kwa vipindi virefu kuliko mwingine.
Kabla ya kutangazwa mshindi, Zungu aliulizwa maswali wakati akijinadi juu ya kipi anakwenda kutenda mara atakapopata nafasi hiyo hasa kwenye suala la kutenda haki.
Mbunge mteule wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu amemuuliza Zungu kipi atakachofanya ikiwemo kutoa nafasi ya wabunge katika kuikosoa Serikali na kutoa usawa kwa wabunge wote ndani ya jengo hilo.
Mbunge mteule wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ameuliza iwapo Spika ataendelea kutumia farsafa yake ya jaza ujazwe.
Akijibu maswali hayo kabla ya kutangazwa mshindi, Zungu amesema kwenye uongozi wake msaafu wake utakuwa ni kanuni za Bunge na Katiba ya nchi na kwamba hatafanya jambo lolote kinyume na hapo.
Kingine ambacho amekiahidi kwa Wabunge ni kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025/2050 ili kuleta haki na kuwasaidia Watanzania kufikia malengo yake.
Hata hivyo, Zungu amesema Bunge na Serikali siyo maadui na hivyo hakuwezi kuwa na msuguano lakini kila mhimili utapaswa kusimama na kwa nafasi yake ili lengo la kuwapa huduma wananchi liweze kufikiwa.
Zungu ameshinda kiti hicho akitokea kuwa Naibu Spika wa Bunge la 12 ambalo Spika wake alikuwa ni Dk Tulia Ackson (Mbunge wa Uyole) ambaye naye aligombea lakini dakika za mwisho aliamua kujitoa.
Maspika wastaafu ni, Dk Tulia Ackson, Job Ndugai, Anne Makinda, Samuel Sitta, Pius Msekwa, Adam Mkwawa na Erasto Mang’enya.