Prime
Zifahamu sababu wasichana kuanza ngono mapema

Dar es Salaam. Wakati wataalamu wakieleza hatari ya msichana kuanza ngono mapema, wadau wa masuala ya kijamii wametaja sababu zinazochangia hali hiyo, ikiwamo ufukara wa familia na malezi mabovu.
Imeelezwa wazazi kukosa muda na watoto wao ni jambo linalochangia baadhi ya ndugu, zaidi wakitajwa wajomba kuanza kuwaingilia kimwili mabinti.
Hayo yanaelezwa wakati Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria ya mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ikionyesha msichana mmoja kati ya 11 huanza ngono kabla ya kufikisha miaka 15, huku mmoja kati ya 34 wakiwa kwenye ndoa.
Kulingana na utafiti huo, hakuna mvulana chini ya miaka 15 aliyeingia kwenye ndoa, lakini msichana mmoja kati ya 100 alijifungua kabla ya miaka 15, huku mmoja kati ya 42 akibeba ujauzito.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Samia Suluhu Hassan, imeandaliwa na NBS kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Mtaalamu wa afya
Akizungumzia hatari ya kuingia kwenye ngono katika umri mdogo, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama katika Hospitali ya Aga Khan, Munawar Kaguta aliiambia Mwananchi kuwa, msichana kuanza ngono mapema huchangia hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
“Hii ni kwa sababu shingo ya kizazi haitakuwa vizuri, pia akipata mimba na nyonga haikukomaa anaweza kujifungua kwa upasuaji au kuchanika wakati wa kujifungua, hivyo anaingia kwenye hatari ya kupata fistula,” alisema Kaguta.
Alisema hata kisaikolojia ipo hatari inayoweza kutokea, hasa mtoto anapolia, msichana ambaye ni mama naye anaweza kulia.
Alisema kitaalamu umri sahihi wa kuzaa ni kuanzia miaka 20 na kuendelea kwa kuwa via vya uzazi huwa tayari vimekomaa.
Athari pia zinazungumzwa na mwanaharakati wa masuala ya ukunga na uuguzi, Martha Rimoy akisema msichana anayejihusisha na ngono akiwa na umri mdogo hupata tatizo la kifafa cha mimba, kutokwa damu nyingi wakati wa kujifunga na unyanyapaa.
“Unyanyapaa unatokea kwa sababu mzazi hakuwa tayari kumuona mtoto wake akiwa na mimba, hivyo jamii inaanza kumnyanyapaa. Watoto hawa wako shuleni, hii ni sawa na mtoto kumbeba mtoto,” alisema Rimoy.
Alisema hata wakati mwingine damu inaweza kutoka ndogo, lakini madhara yakawa makubwa kutokana na wasichana hao kutohudhuria kliniki inavyotakiwa kwa kukosa ushirikiano kwenye jamii.
Sababu nyingine ni kukosa usafiri na kufukuzwa nyumbani baada ya kupata ujauzito.
“Namna nzuri ya kukabiliana na ngono mapema kwa watoto ni wazazi kuwajibika, waangalie watoto wanafanya nini ili pale anapokwenda kinyume wamkanye haraka, jamii iwaachie watoto wa kike wasome, wasiwaharibie maisha yao. Wizara ndani ya Serikali zishirikiane kukabili tatizo hili,” alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania, Jane Maira, alisema sababu ya wasichana kuingia kwenye ngono wakiwa na umri mdogo ni ufukara ndani ya familia.
Alisema watoto wanashindwa kumudu mahitaji, hivyo kuingia kwenye mtego wa kuanza ngono mapema ili kupata fedha za kununua taulo wakati wa hedhi.
“Mtoto anaposhinda shuleni bila kula na hakutoka hata na fedha kidogo nyumbani, kadiri anavyopevuka anaona wenzake wanapata fedha kwa njia zisizo sahihi naye huona ni kawaida,” alisema.
Akizungumzia kundi rika, alisema ni tatizo lingine kwa watoto kuanzia miaka tisa hadi 15 ambao huingia kwenye makundi yasiyo sahihi.
“Jambo lingine linalowatumbukiza wasichana kwenye ngono mapema ni migogoro baina ya wazazi. Mama anakwenda upande wake, baba wake na mtoto anakaa kwa mzazi mmoja au kwa ndugu. Mazingira haya humpa changamoto, hajui amuombe nani msaada, hivyo inakuwa rahisi kuingia kwenye ngono mapema,” alisema.
Katika kukabiliana na hilo, alishauri kuundwa klabu za elimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi shuleni, akisema zitapunguza ngono za mapema na madhara ya ndoa za utotoni.
Alisema ni muhimu kwa wazazi kuwa makini wanapowapeleka watoto kwa wajomba au kuwaachia ndugu kwa kuwa maadili yameporomoka, watoto wadogo huingiliwa kimwili na ndugu zao.
Mhadhiri mtaalamu wa masuala ya ustawi wa jamii, Dk Zena Mnasi, alisema mbinu ya kukabili tatizo hilo ni kujua chanzo cha wasichana kuingia kwenye ngono.
Alisema ukaribu wa baba na mama kwa watoto umekuwa mdogo, hivyo anapopitia changamoto hukosa msaada wa haraka.
“Watoto waepushwe na matumizi mabaya ya mitandao kwa sababu maovu wanayoona wanakwenda kuyajaribu. Jamii iwe na jukumu la kulinda usalama wa watoto, wapewe elimu ya kujikinga na ngono kwenye umri mdogo,” alisema.