Wizi wa dira za maji wazidi kushamiri, wafanyabiashara wahadharishwa

Baadhi ya vifaa ikiwemo Dira za maji zinazodaiwa kuibwa na watu wasiojulikana kutoka kwenye miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Kahama (Kuwasa). Picha na Amina Mbwambo
Muktasari:
- Kuanzia kipindi cha Oktoba 2024, hadi Aprili 2025, jumla ya dira za maji 210 zenye thamani ya zaidi ya Sh25.2 milioni, mali ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (Kuwasa) zimeibwa katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga na kusababisha hasara kwa wananchi na mamlaka hiyo.
Kahama. Wimbi la wizi wa dira za maji katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, limeendelea kushika kasi tangu Oktoba 2024 hadi Aprili 2025.
Katika kipindi hicho, jumla ya dira 210 zenye thamani ya zaidi ya Sh25.2 milioni mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (Kuwasa), zimeripotiwa kuibwa.
Taarifa zinaeleza Kuwasa imelazimika kusitisha huduma kwa baadhi ya wateja wake ili kuhudumia waliopoteza dira, hali inayorudisha nyuma juhudi za upatikanaji wa maji kwa wakazi wa maeneo husika.
Hadi sasa haijafahamika wazi dira hizo hupelekwa wapi wala hutumika kwa kazi gani.
Katika juhudi za kudhibiti wizi huo, operesheni ya pamoja kati ya Kuwasa, Jeshi la Polisi na wananchi ilimnasa Rajabu Masimbe, mfanyabiashara wa vyuma chakavu na mkazi wa mtaa wa Mhongolo, akiwa na dira mbili za maji mali ya mamlaka hiyo, kinyume na utaratibu.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Aprili 24, 2025, Masimbe amedai kuwa dira hizo zilifikishwa kwake na vijana wanaokusanya vyuma mtaani mnamo Aprili 23, ambapo zilipokelewa na kijana wake ambaye alizipima bila kuzifanyia ukaguzi.
“Nilikuta tayari zimenunuliwa na kijana wangu, ambaye alizipokea bila kuchunguza yaliyomo kwenye mifuko. Sijui nani aliyeleta, maana huwa napokea vyuma kutoka kwa watu mbalimbali wa mtaani,” amesema Masimbe.

Ofisa Mahusiano wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Kahama (Kuwasa) John Mkama (kulia), akikagua Dira zinazodaiwa kuwa mali ya Kuwasa, ambazo ziliibwa na watu wasiojulikana na kukutwa kwa mfanyabiashara wa vyuma chakavu na plastiki Rajabu Masimbe (kushoto). Picha na Amina Mbwambo
Wakazi wa Kahama, akiwamo Shakira Mohamed, wameeleza masikitiko yao juu ya wizi huo, wakisema umeathiri upatikanaji wa huduma ya maji.
“Hali ni ngumu. Ukifika Kuwasa unaambiwa ununue dira mpya. Huna pesa, unabaki bila maji. Serikali ichukue hatua,” amesema Shakira.
Sharif Saidi ameitaka Serikali kuwachunguza wafanyabiashara wa vyuma chakavu, na kuchukua hatua kali dhidi ya wanaopatikana na vifaa vya Serikali, akiamini hatua hiyo itapunguza wizi na hasara kwa wananchi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale, amethibitisha tukio hilo kutokea katika mtaa wake na kusema matukio ya wizi wa dira na koki za maji yamekithiri.
Amewaonya wafanyabiashara wa vyuma kujiepusha na ununuzi wa nyara za Serikali.
Ofisa Uhusiano wa Kuwasa, John Mkama amesema wizi wa dira za maji ni changamoto kubwa kwao.
Amesema usiku wa kuamkia sikukuu ya Pasaka, Aprili 20, 2025, dira nane ziliibwa katika eneo la Malunga, hali iliyosababisha hitilafu kubwa ya huduma.
Mkama amezitaja kata za Nyahanga, Malunga, Majengo na Mhongolo kuwa miongoni mwa zilizoathirika.
Amesema mamlaka hiyo iliitisha kikao na wafanyabiashara wa vyuma chakavu na kuwapa maelekezo ya kujiepusha na ununuzi wa vifaa vya mamlaka hiyo, lakini juhudi hizo hazijazaa matunda.

Eneo la mfanyabiashara wa vyuma chakavu na plastiki Rajabu Masimbe lililopo mtaa wa Mhongolo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, zinapodaiwa kukutwa Dira mbili na koki za maji, mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (Kuwasa). Picha na Amina Mbwambo
“Changamoto hii imekuwa kubwa tangu mwaka 2024. Hasara ni kubwa kwa mamlaka, na pia kwa wananchi ambao hukosa huduma kwa muda mrefu,” amesema Mkama.