Wenyeviti Serikali za mitaa watwishwa zigo ulinzi miundombinu ya Tanesco

Muktasari:
- Uongozi wa Serikali za mitaa una nafasi kubwa katika kulinda miundombinu ya Tanesco, utoaji huduma pamoja na mawasiliano kati ya shirika hilo na wananchi.
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limewapa uongozi wa serikali za mitaa wakiwemo wenyeviti na watendaji jukumu la kuwaunganisha wananchi na shirika hilo katika utoaji huduma na mawasiliano.
Sambamba na hilo viongozi hao wametwishwa jukumu la ulinzi wa miundombinu ya shirika hilo ikiwemo nguzo, nyaya, transfoma na mingine ya kusafirisha umeme kwa kuwa wako karibu na jamii ambayo ndiyo inapewa huduma hiyo muhimu ya kiuchumi.
Hayo yamejiri leo Juni 24, 2025 kwenye kikao kazi cha Shirika la Tanesco na wenyeviti wa Serikali za mitaa Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo kilichofanyika Ubungo Plaza Dar es Salaam kilichohudhuriwa na uongozi wa mkoa, Wilaya za Ubungo na Kinondoni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Imeelezwa uongozi wa mtaa una jukumu muhimu la kusimamia na kuzuia uhalifu wa kuharibu miundombinu ikiwemo waiba mafuta ya tansfoma, nyaya.
Pia, wanalo jukumu la kusaidia shirika kupokea maoni ya wananchi kupitia taarifa mrejesho kwa shirika.
Akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema wenyeviti wa mitaa wanakuwa mabalozi wa huduma za umeme ambapo watatoa taarifa za huduma wanazopatiwa na shirika hilo.
“Tanesco inawajibu wa kuhudumia wateja wetu wengi na msingi wa huduma hizo ni mawasiliano ndio maana tuna kituo cha huduma kwa wateja ikiwa ni juhudi za kuwasiliana na wateja.
“Lakini hilo pekee halitoshi bado tunahitaji mfumo mzuri wa mawasiliano na wenyeviti wa Serikali za mitaa ndio maana tunataka tujue wananchi wanasemaje kupitia ninyi,” amesema.
Amesema lengo la Tanesco ni kutengeneza urafiki kati ya shirika wenyeviti na wananchi waone namna huduma zinavyotolewa na kupata taarifa ya mwitikio ya kazi hizo.
Aidha, Mkurugenzi amesema wenyeviti wanapaswa kutambua endapo mtu akiharibu miundombinu basi atasababisha kutopatikana na huduma.
Akisisitiza juu ya ulinzi wa miundombinu mgeni rasmi wa kikao kazi hicho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema umeme ni uhai kama ilivyo maji hivyo haina budi kulindwa ambapo jukumu hilo linaanzia kwa uongozi wa Serikali za mtaa.
Akitolea mfano, amesema transfoma ikiibwa maana yake huduma haitapatikana na amani itatoweka. Wenyeviti wanapaswa kujua wakiona mtu anaharibu au anaiba miundombinu ya Tanesco wanapaswa kufahamu ni kielelzo cha kuhatarisha amani.
“Tunataka ushirikiano kwa sababu umeme ni ajira na kuna watu wamejiari, umeme ni maisha kuna watu wanatumia mashine za oksijeni kupumua, umeme ni pato la taifa, kama wanavyosema maji ni uhai basi na umeme pia ni uhai,” amesisitiza Chalamila.
Chalamila amesema utekelezaji wa miradi ya Tanesco unafanyika kwenye Serikali za mitaa ambapo kuna wananchi moja kwa moja kwa namna hiyo Wenyeviti ni watetezi wa ulinzi wa amani, miundombinu ikiwemo hiyo ya Tanesco.
Wanaoharibu miundombinu tutakula nao sahani moja
Akizungumza na Mwananchi nje ya kikao hicho Mwenyekiti wa Wenyeviti Wilaya ya Kinondoni, Lazarus Mwakiposa amesema miundombinu ya Tanesco inahitaji kusimamiwa ili isiharibiwe na jukumu hilo analisimamia vyema.
“Wale wote wanaoiba kopa, mafuta na miundombinu mingine tutakula nao sahani moja kwa maana tukimkamata tunampeleka ashitakiwe na sheria itachukua mkondo wake,” amesema Mwakiposa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti Mtaa wa Kimamba Kata ya Makulumla Wilaya ya Ubungo, Abdallah Mchela amesema wale wote wasio wazalendo kuchezea miundombinu ya umeme watashughulikiwa.
Katika hatua nyingine imetolewa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupitia ya umeme ili kuendana na kasi ya kampeni ya Serikali ya kuhimiza matumizi ya nishati safi hadi ifkapo mwaka 2034.
Katika kikao kazi hicho, imelezwa jiko la umeme unaweza kutumia chini ya uniti moja ukapika chakula kwani ni nishati yenye gharama nafuu.