Wenye ulemavu kukutanishwa Kilimanjaro

Rais wa shirika la New life foundation, Askofu Mstaafu wa TAG, Askofu Glorious Shoo akizungumzia kongamano litakalowakutanisha wenye ulemavu Mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Shirika lisolikuwa la kiserikali la New Life Foundation, mkoani Kilimanjaro limeandaa hafla ya siku moja ya kuwakutanisha watu wenye ulemavu ili kuonyesha jamii kuwa wanapaswa kuheshimiwa kama ilivyo kwa watu wengine.
Moshi. Shirika lisolikuwa la kiserikali la New Life Foundation, mkoani Kilimanjaro limeandaa hafla ya siku moja ya kuwakutanisha watu wenye ulemavu ili kuonyesha jamii kuwa wanapaswa kuheshimiwa kama ilivyo kwa watu wengine.
Hafla hiyo iliyopewa jina la 'The night to shine' itawakutanisha wenye ulemavu zaidi ya 60 mkoani hapa Februari 9, ambapo siku hiyo itakuwa ni siku ya kipekee kwao kwa kuwa watavalishwa mataji maalumu pamoja na kubadilishana mawazo.
Akizungumzia shughuli hiyo jana mjini hapa Februari 8, Rais wa Shirika hilo, Askofu mstaafu wa TAG, Glorious Shoo, amesema lengo la kuwakutanisha watu hao wenye ulemavu ni kuwawekea kumbukumbu ya upendo katika maisha yao.
"Tumekusudia kufanya jioni hii ambayo tunawaleta kwa pamoja wenzetu ambao wana ulemavu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kuweza kuwaonyesha tunawatambua, kuwathamilini na tunawaona ya kwamba wanapaswa kuheshimiwa na kupewa kipaumbele kama ilivyo kwa watu wengine," amesema Shoo.
Amesema usiku huo ambao wameuandaa maalumu kwa ajili ya wenye ulemavu watavalishwa taji maalum kwa kuonyesha kuwa jamii ina waheshimu na kuwathamini na kwamba mtu yeyote anaweza kuwa ni mlemavu ajaye.
"Lengo kubwa ni kuendelea kuikumbusha jamii kwamba mimi na wewe kesho tunaweza kuwa na ulemavu au kukaa kwenye kiti kile ambacho mlemavu amekikalia.
"Tunapenda kuwaalika watu binafsi, watu mbalimbali, vikundi ambavyo vingependa kushirikiana nasi katika tukio hili kwa ajili ya kufanikisha siku hii," amesema.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo na uwezeshaji wa shirika hilo, Gerald Simon, amesema pamoja na kufanya sherehe hiyo maalum kwa wenye umelavu jamii inakumbushwa kufanya wajibu wake wa kuhakikisha inawakumbuka wenye mahitaji maalum.
"Tutatoa viti mwendo kwa wale wenye mahitaji maalum lakini tunaendelea kuangalia mahitaji yao ambayo taasisi tungeweza kufanya kwa kiasi chake lakini kuonyesha jamii wajibu wa kuilea na kuikumbuka,"
"Wapo baadhi ya wenye ulemavu ambao wamefichwa nyumbani wapo wengine wamefika umri wa kwenda shuleni lakini hawakupelekwa,” amesema.