Waziri aagiza mtendaji, mwenyekiti wa kijiji kukamatwa

Mariamu Mgunda ambaye ni mtendaji wa kijiji cha Nyamlilio wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza pamoja na mwenyekiti Mateso Shibayi
Muktasari:
- Waziri wa Tamisemi Ummy Mwalimu ameagiza kukamatwa na kuwasimamishwa kazi watendaji wawili akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamlilio wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, kwa madai ya kuwachangisha wananchi kwa nguvu fedha za maendeleo.
Sengerema. Waziri wa Tamisemi Ummy Mwalimu ameagiza kukamatwa na kuwasimamishwa kazi watendaji wawili akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamlilio wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, kwa madai ya kuwachangisha wananchi kwa nguvu fedha za maendeleo.
Viongozi hao ni Mariamu Mgunda ambaye ni mtendaji wa kijiji hicho pamoja na mwenyekiti Mateso Shibayi.
Agizo hilo amelitoa leo Jumamosi Agosti 14, 2021 baada ya wananchi kulalamikia mambo wanayofanyiwa na viongozi hao ikiwamo kukamata mifugo kwa kushindwa kutoa mchango.
Baada ya malalamiko hayo, Ummy ameagiza watendaji wote wa vijiji na kata nchi nzima wasichangishe fedha kwa wananchi bila kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya husikia.
Mkazi wa Kijiji cha Nyamililo, Sijali Matias amedai kuwa Machi 18 mwaka huu, mtendaji na mwenyekiti huyo walifika nyumbani kwake wakachukua mbuzi jike.
Amesema baada ya siku tano alikwenda ofisi ya mtendaji na Sh30,000 kwa ajili ya kuchuku mbuzi wake lakini kitendo kilichofanyika alikosa amani.
Akijibu malalamiko hayo, mtendaji Mariamu Mugunda amesema michango hiyo walikubalina na wananchi kupitia vikao vyote vya kijiji hicho na hajaenda kinyume na utaratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriey amesema atafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo na atakayebainika atafikishwa Mahakamani.