Wawili wafa maji ziwa Victoria

Muktasari:
- Wavuvi wawili katika mwalo wa Bunyorwa kando ya ziwa Victoria katika wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu wamefariki dunia baada ya kuzama maji wakati wanavua samaki.
Busega. Wavuvi wawili katika mwalo wa Bunyorwa kando ya ziwa Victoria katika wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu wamefariki dunia baada ya kuzama maji wakati wanavua samaki.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Septemba 22, 2022 na kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, Bladius Chatanda imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Septemba 18, 2022 saa mbili usiku wakati wavuvi hao walipokumbwa na dhoruba ya upepo.
Katika taarifa hiyo Chatanda amewataja waliofariki kuwa ni Ntambi Swilila (32) mkazi wa kijiji cha Kahangalala wilaya ya Busega na Deus Ntandila (56) mkazi wa kijiji cha Mwanegeyi wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza.
"Miili imepatikana septemba 20 na baada ya uchunguzi wa kitabibu ilikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi, katika mtumbwi walikuwepo wavuvi wanne na wawili kati yao waliokolewa".
Chatanda amewataja manusura wa ajali hiyo kuwa ni Isacka Masigani (20) mkazi wa kijiji cha Kitongo wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza na Sahani Simba (21) mkazi wa kijiji cha Masanza wilaya ya Busega ambao waliokolewa na wavuvi wenzao waliofika eneo la tukio kutoa msaada.
Aidha jeshi hilo la polisi limetoa wito kwa wavuvi wote wanaofanya shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria kwa mialo iliyoko katika mkoa huo, kuchukua tahadhari wakiwa kwenye shughuli zao kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa ili kupunguza madhara yatokayoweza kugharimu maisha na mali za Wavuvi.