Wawili kortini wakidaiwa kughushi nyaraka za ardhi na mirathi
Mfanyabiashara Betha Laurence, akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka yao .
Muktasari:
- Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Aprili 18, 2008 Desemba Mosi 2009 na Agosti 21, 2015, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara Seleman Said na Betha Laurence wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 16, yakiwemo ya kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za uongo na utakatishaji wa mali.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Juni 5, 2026 na mashtaka dhidi yao yamesomwa na Wakili wa Serikali, Geofrey Olugwey, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ya kughushi nyaraka na sita ya kuwasilisha nyaraka za uongo.
Aidha, Said anakabiliwa na shtaka moja la kushiriki ukaguzi wa nyaraka hizo na kujipatia usajili wa ardhi kwa njia ya udanganyifu, pamoja na shtaka la utakatishaji wa fedha.
Olugwey alidai kuwa Aprili 18, 2008, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walighushi mkataba wa mauziano kwa lengo la kuonyesha kuwa Seleman Said alinunua kiwanja namba 212 kilichopo Kinondoni kwa Sh20 milioni, huku wakijua taarifa hizo si za kweli.
Pia, wanadaiwa kughushi kiapo kilichoonyesha kuwa Ramadhani Mussa, Rehema Mussa, Mwanahamisi Mussa na wengine walikubali kumuuzia kiwanja hicho.
Nyaraka nyingine zinazodaiwa kughushiwa ni fomu za mirathi namba moja, mbili, tatu na nne zinazomhusu marehemu Mussa Kondo Majenga.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Said aliwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Romanus Sanda, kwa lengo la kupata usajili wa ardhi.
Aidha, inadaiwa kuwa akiwa na maofisa wengine wa ardhi, Said alishiriki ukaguzi wa nyaraka hizo zilizotumika kusajili ardhi na hatimaye kupata hati ya ardhi namba 1003 kwa jina lake.
Mfanyabiashara Seleman Said, akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka yao .
Katika shtaka jingine, Said anadaiwa kuwa Juni 27, 2008, akiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wilayani Ilala, alijipatia hati ya umiliki wa ardhi namba 105525 kutoka kwa Msajili wa Ardhi kwa kujifanya kuwa alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Moshi Majenga, huku akijua si kweli.
Pia, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 1, 2009 na Agosti 21, 2015, alitoa ushahidi wa uongo katika Shauri la Ardhi namba 62 la mwaka 2019 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, akidai kuwa alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Moshi Majenga.
Said pia anakabiliwa na shtaka la utakatishaji wa fedha akidaiwa kuwa Agosti 1, 2008, alijipatia ardhi hiyo huku akijua ilitokana na kosa tangulizi la kughushi nyaraka.
Baada ya kusomwa mashtaka hayo, Betha aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
Said alipelekwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji wa fedha kutokuwa na dhamana.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18, 2026, itakapotajwa tena mahakamani.