Mtunza stoo kortini akidaiwa kumuibia mwajiri wake Sh88 milioni
Mshtakiwa Saqlain Jalali, akiwa chini ya ulinzi wa askari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa yake, kati ya Desemba Mosi, 2024 na Septemba 25, 2025, eneo la Buza, wilaya ya Temeke.
Dar es Salaam. Mtunza stoo wa Kampuni ya Emperial Road Haulage Limited, Saqlain Jalali (28) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni wizi akiwa mtumishi na utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh88 milioni, mali ya mwajiri wake.
Jalali ambaye ni mkazi wa Kariakoo Wilaya ya Ilala, amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 6, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 9599 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Lema.
Lema amemsomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Akisomewa mashtaka yake, wakili Lema alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la wizi akiwa mtumishi tukio a alodaiwa kulitenda kati ya Desemba 1, 2024 na Septemba 25, 2025 eneo la Buza, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Ilidaiwa, katika tarehe hizo, mshtakiwa akiwa mtunza stoo wa kampuni hiyo, aliiba Sh88,764,871 mali ya kampuni hiyo.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha, shtaka analodai kulitenda siku na eneo hilo, ambapo Jalali akiwa mtunza stoo wa Kampuni hiyo, alijipatia kiasi hicho wakati akijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la wizi akiwa mtumishi.
Baada ya kumaliza kusomewa mashtaka yake, mshtakiwa hakutakuwa kujibu chochote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya Uhujumu uchumi.
Mshtakiwa Saqlain Jalali, akiwa chini ya ulinzi wa askari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi. Picha na Hadija Jumanne
Vilevile shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana, hivyo atapelekwa rumande.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai, upelelezi haujakamilika hivyo kesi imeahirishwa hadi Mei 18, 2026 itakapotajwa na mshtakiwa amepelekwa rumande.
Wakati huo huo, wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Hekima Mwasipu ameieleza mahakama hiyo kuwa mteja wake anania ya kuingia katika makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ya kukiri kosa na kuimaliza kesi hiyo.
Mwasipu ametoa taarifa hiyo, muda mfupi baada ya upande wa Jamhuri kumsomea mshtakiwa mashtaka yake.
Mwasipu amedai kuwa ataandika barua na kuwasilisha sehemu husika.