Mfanyabiashara kortini akidaiwa kujipatia Sh120 milioni kwa udanganyifu
Mshtakiwa Abdul Ahmed, akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya jinai. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 2, 2023 mtaa wa Nyamwezi uliopo Kariakoo wilaya ya Ilala, akiwa mfanyabiashara alijipatia Sh120 milioni, ambazo zilikuwa kwa ajili ya ununuzi wa dola za Marekani
Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Abdul Razak Ahmed (37) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la kujipatia Sh120 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Ahemd, mkazi wa Ilala mtaa wa Arusha, anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Tamimu Maruhuni kwa ajili ya ununuzi wa dola za Marekani 50,000, lakini hakufanya hivyo.
Mshtakiwa huyo amefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi Mei 21, 2026 na kusomewa kesi ya jinai namba 11008 ya mwaka 2026.
Amesomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling'i, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Bilal Ahmed.
Wakili Mbiling'i alidai mshtakiwa anadaiwa Mei 2, 2023 katika mtaa wa Nyamwezi iliyopo Kariakoo wilaya ya Ilala, akiwa mfanyabiashara na kwa makusudi alijipatia Sh120milioni kutoka kwa Tamimu Maruhuni.
"Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hiyo kwa ajili ya ununuzi wa dola za Marekani 50,000, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli," amesema wakili Mbiling'i.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi bado haujakamilika, hivyo waliomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu amemueleza mshtakiwa kuwa shtaka linalomkabili lina dhamana na kisha kutoa masharti matatu ya dhamana.
Sharti la kwanza, mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa au taasisi inayotambuliwa kisheria.
Pia wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida) na mmoja kati ya wadhamini hao anatakiwa kuweka fedha taslimu Sh60 milioni au kukabidhi mahakamani hapo mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Sharti la tatu, wadhamini hao kila mmoja wanatakiwa kusaini fungu la dhamana ya ahadi ya maneno yenye thamani ya Sh20 milioni.
Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande hadi Juni 3, 2026 kwa kutajwa.