Watu 500 kushiriki mkutano maalumu baraza la vyama vya siasa

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ally Ahmed
Muktasari:
- Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ally Ahmed, amesema jumla ya wadau 500 watashiriki mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau demokrasia wa vyama vingi.
Dar es Salaam. Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ally Ahmed, amesema jumla ya wadau 500 watashiriki mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau demokrasia wa vyama vingi.
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 11 hadi 13 mwaka huu na utafunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku siku ya mwisho hotuba itatolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi.
Mkutano huo si wa kwanza kufanyika kwani Desemba 15 hadi 17, 2021; ulifanyika mkutano kama huo jijini Dodoma, ambao ulifunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambao kimsingi ndiyo chanzo cha kuliundwa na kikosi kazi ambacho kilikuwa kinaratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Akizungumza Dar es Salaam katika mkutano wake na vyombo vya habari leo Septemba 9,2023, Mohammed ameeleza kuwa shabaha ya mkutano huo ni kupokea taarifa ya kikosi kazi na kufanya tathmini kwa kuangalia ni mambo gani yameshafanyiwa kazi na ambayo hayajafanyiwa kazi.
"Kupitia mkutano huo wadau watapata fursa ya kutoa maoni yao na kujadili kasi iliyotumika hadi walipofikia na jambo gani linapaswa kufanyika kwa kutoka maazimio katika mkutano huo," amesema.
Akizungumza kama mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo, Ahmed amesema mada nyingine itakayojadiliwa na wadau hao ni kuangalia hali ya kisiasa.
"Kauli mbiu ya mkutano huu itakuwa ni 'Imarisha Demokrasia Tunza Amani yetu'," amesema.