Rais Samia kufungua mkutano wa wadau wa vyama vya siasa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Disemba 15, 2021 atafungua mkutano wa wadau wa vyama vya siasa nchini ambao unalenga kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
Dodoma. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Desemba 15, 2021 atafungua mkutano wa wadau wa vyama vya siasa nchini ambao unalenga kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika jijini Dodoma umeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni, Zitto Kabwe (Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo), na wenyeviti wa vyama Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Augustino Mrema (TLP), Hashim Rungwe (Chauma), John Shibuba (ADA-TADEA) John Cheyo (UDP) na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama Cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, wenyeviti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa na Zanzibar, Jeshi la Polisi, Spika Mstaafu Anne Makinda, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba.
Vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi havikuhudhuria mkutano huo huku wakitaja sababu za kutohudhuria ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa na uhuru na kuzuiwa wa mikutano ya kisiasa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa mkutano huo utahudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na wadau wa vyama tangu aapishwe kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano John Magufuli