Watoto watatu familia moja wafa maji wakivua mtoni

Katavi. Watoto watatu wa familia moja Lucia Lazima (10), Kabisi Lazima (8), na Makala Lazima (6), wakazi wa Kitongoji cha Kayenze B wilayani Mpanda, wamekufa maji wakati wakivua samaki Mto Kamilala.

Watoto hao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kamilala ambapo Lucia alikuwa anasoma darasa la tano, Kabisi darasa la nne na Makala darasa la kwanza.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, akizungumza na wanahabari leo Julai 19, 2023 amesema tukio hilo limetokea Julai 13, 2023 saa 7:45 mchana.

“Eneo la mto huo linatumika pia kwa shughuli za uvuvi samaki, watoto hao walikwenda kuvua samaki, haikufahamika kama walikuwa wanaogelea au ilikuwaje,” amesama kamanda huyo na kuongeza;

“Kwa sababu miili yao ilikutwa ikielea na wasamalia wema wakatoa taarifa polisi, ikaopolewa na kufanyiwa uchunguzi kisha ndugu wakakabidhiwa kwaajili ya taratibu za maziko,” amesema Ngonyani.

Kamanda Ngonyani ametoa rai kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu pindi watoto wao wanapotoka nyumbani kwenda kujitafutia kipato.

Katika tukio lingine Ramadhan Pongera (85) mkazi wa Kitongoji cha Uvuvi, Kijiji cha Katambike, wilayani Mpanda, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumjeruhi tumboni Meshack Binari (35), na kitu chenye ncha kali.

Chanzo cha tukio hilo lilitokea Julai 13,2023  kinatajwa kuwa mhanga ambaye kwa sasa ni marehemu, kumzuia mtuhumiwa kuingia katika chumba cha jirani yake ambaye ni Mariam, akidaiwa kuwa na lengo la kumwingilia kimwili bila ridhaa yake.

“Baada ya marehemu kuchomwa, alikimbizwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi na kupatiwa matibabu lakini Julai 14, 2023 alifariki, mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” amesema.

Wakati huo huo mtu mmoja anayedhaniwa kuwa mchimbaji madini katika mgodi wa mlima Dilif Wilaya ya Mpanda, anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mtoto (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu, jina la shule imehifadhiwa.

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa alimvizia mhanga wakati anapita njiani vichakani akamfanyia kitendo hicho cha kikatili.

“Wazazi walitoa taarifa polisi mhanga aliandikiwa PF3 akapelekwa hospitali kutibiwa na kwamba kwa sasa anaendelea vizurina ameruhusiwa kurudi nyumbani,” amesema Kamanda huy na kuongeza;

“Mhanga tulivyomhoji anasema anamtambua kwa sura japo jina hamfahamu tunaendelea kumtafuta ili tumkamate,” amesema Ngonyani.

Pia watu wawili wamefikishwa mahakamani baada ya kukamatwa wakiwa na madawa ya kulevya aina ya bangi kilogramu 12 na kete 144.

Watuhumiwa hao ni Jafary Rashid (26) na Bahati Masanja (30) ambapo upelelezi unaendelea na sampuli ya madawa hayo imechukuliwa imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali kufanyiwa uchunguzi.

“Uchunguzi ukikamilika tunawafikisha mahakamani lakini tumewakata watuhumiwa wengine zaidi ya 10 wanatuhumiwa kwa wizi wa vitu tofauti kama vile televisheni, redio, meza, spika za redio, simu ya mezani, solar, feni, baiskeli na vipande 15 vya nondo wanavyotumia kwenye uhalifu,”amesema Ngonyani.

Kwa mujibu wa Kamanda Ngonyani watu wanaojihusisha na uhalifu ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia watakamatwa na wataadabishwa kwa mujibu wa sheria.