Prime
Watoto wanavyobebeshwa mzigo wa vita vya wazazi
Muktasari:
- Wataalamu washauri jamii kujenga utamaduni wa kutenganisha migogoro ya watu wazima na haki ya watoto, ili kuwalinda dhidi ya taarifa ay mazingira yanayoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.
Dar es Salaam. Matukio ya baadhi ya wanawake wanaodaiwa kuwahusisha wanaume zaidi ya mmoja na kila mmoja kumwaminisha ni baba wa mtoto, yametajwa kuwa chanzo cha migogoro yenye athari kubwa maishani.
Katika siku za karibuni, mijadala kuhusu baadhi ya wanawake wanaodaiwa kuwa na uhusiano na wanaume zaidi ya mmoja na baadaye kuibuka sintofahamu kuhusu baba halali wa mtoto, imezua mjadala mpana kwenye familia nyingi na mitandao ya kijamii na mara nyingine imesababisha vifo.
Ingawa matukio ya aina hiyo yamekuwa yakivuta hisia za wengi na kuzua mijadala mikali mitandaoni, wataalamu wa saikolojia, sheria na familia wanaonya kuwa nyuma ya mjadala huo kuna mtoto ambaye anaweza kuathirika moja kwa moja kisaikolojia, kijamii na kihisia, hasa pale anapowekwa katikati ya mashindano ya wazazi au familia zao.
Onyo hilo linakuja kukiwa na matukio ya wazazi kugombea watoto kwa kile kinachodaiwa mama kutoa taarifa kwa watu tofauti kuhusu baba halali wa mtoto, huku wengine wakichagua kumwaga masuala ya familia mbele ya umma wakiamini watapata uungwaji mkono au haki.
Mfano wa hilo ni tukio la hivi karibuni ambapo kijana mmoja alijitokeza akidai kunyimwa haki ya kuwa baba wa mtoto anayeamini alizaa na mbunifu wa mitindo, huku mbunifu huyo akijitokeza na kukiri kweli alikuwa na uhusiano na kijana huyo lakini ujauzito haukuwa wake licha ya kumhusisha nao hapo awali.
Juni 1, 2026 akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Kigoma Mjini, Baba Levo alisema baadhi ya wanaume hukumbana na changamoto kubwa wanapogundua baada ya muda mrefu kuwa watoto waliokuwa wakiwalea si wao wa kibaolojia.
“Huwezi kuishi na mwanamke ndani, anakusingizia ujauzito, unauelea miezi tisa hadi anapojifungua na unamlea mtoto hadi anafika miaka 10. Hapo inapotokea ugomvi kidogo anakwambia mtoto huyo si wako,” alisema.
Amesema katika mazingira hayo mwanaume anaweza kuchukua hatua mbalimbali za kisheria au kutafuta ukweli, lakini baadhi yao wanaweza kushindwa kudhibiti hisia zao na kusababisha matukio ya ukatili wa kijinsia.
“Ipo namna ambavyo mwanaume anaweza kuchukua hatua kukabiliana na hilo, lakini kuna wengine wanaweza kukabiliana nalo kwa hasira. Wakati mwanaume anapambana na lile neno aliloambiwa, inawezekana kukatokea ukatili wa kijinsia. Niwasihi wanawake muwe wa kweli kama mtu ujauzito si wake, mwambie ukweli na usimbebeshe mzigo mwanaume ambaye si baba wa mtoto wake,” alisema Baba Levo.
Akizungumzia hilo mkazi wa Kisemvule , Asha Mohamed amesema mtoto hapaswi kuwa sehemu ya mapambano ya wazazi.
“Haijalishi nani yuko sahihi au amekosea, mwisho wa siku mtoto ndiye anayebeba jina na kumbukumbu za mambo haya yote,” amesema.
Naye mkazi wa Temeke, Juma Khamis amesema teknolojia imewafanya baadhi ya watu kutafuta uamuzi wa umma badala ya kutumia njia zinazotambulika.
“Mara nyingi watu wanahukumiwa na maoni ya mitandaoni kabla hata ukweli haujajulikana. Hilo si jambo jema kwa familia wala kwa watoto,” amesema Khamis.
Wasemavyo wanasaikolojia
Pamoja na mitazamo hiyo ya kijamii, Mwanasaikolojia wa jamii, Sabrina Kimiro amesema mwenendo wa baadhi ya watu kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja wakati wa mahusiano, unaweza kuwa chanzo cha migogoro ya muda mrefu, hasa pale mtoto anapozaliwa na ukweli kuhusu ubaba unapokuja kujulikana baadaye.
Amesema migogoro ya aina hiyo haiishii kwa wazazi pekee, huathiri zaidi mtoto anayekuwa katikati ya mgogoro na anaweza kukumbwa na changamoto za kisaikolojia endapo atakua akijua kuwa suala la kuzaliwa kwake limekuwa chanzo cha migogoro kati ya watu waliopaswa kuwa walezi wake.
"Mtoto anahitaji mazingira ya usalama, upendo na ukweli. Pale ambapo wazazi wanakuwa na migogoro inayohusisha suala la utambulisho wake, inaweza kuathiri namna anavyojiona na mahusiano yake baadaye," amesema Sabrina.
Kwa upande wake, mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Vera Malope amesema changamoto hiyo mara nyingi huanzia katika ukosefu wa uaminifu kwenye uhusiano.
"Ukweli katika mahusiano ni msingi wa kujenga familia yenye afya. Kumficha mwenza taarifa muhimu kuhusu mtoto kunaweza kuleta madhara makubwa kwa watu wote wanaohusika," amesema Veronica.
Akizungumzia hilo, mhadhiri wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Hilda Mwakalonge, amesema mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya migogoro ya watu wazima kwa sababu madhara yake yanaweza kudumu kwa muda mrefu.
"Mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya migogoro ya watu wazima. Anapokuwa sehemu ya mjadala wa umma kabla hata ukweli haujathibitishwa, kuna uwezekano wa kukua akiwa na majeraha ya kisaikolojia, kupoteza kujiamini na hata kukumbana na unyanyapaa," amesema Dk Mwakalonge.
Amesema katika zama za mitandao ya kijamii, taarifa zinazowekwa mtandaoni zinaweza kubaki kwa muda mrefu na kumfuata mtoto hata anapokuwa mtu mzima.
"Ni muhimu kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo, usuluhishi au vyombo vya sheria badala ya kuhamisha kila jambo kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa athari zake zinaweza kuwa kubwa kuliko wanavyofikiria," amesema.
Mitandao inapogeuka mahakama
Mtaalamu wa mawasiliano ya kidijitali, Joseph Mallya, amesema mitandao ya kijamii imebadili namna watu wanavyoshughulikia migogoro yao binafsi.
Amesema baadhi ya watu huamini kutoa taarifa hadharani kutawasaidia kupata uungwaji mkono wa jamii, lakini mara nyingi hali hiyo hugeuka kuwa hukumu ya umma kabla ya ukweli kujulikana.
"Watu wengi wanaamini wakizungumza hadharani watapata uungwaji mkono wa umma, lakini mara nyingi mjadala huo hugeuka kuwa hukumu ya mitandao badala ya kutafuta ukweli," amesema.
Amesema tabia ya kurekodi video za kujitetea au kushambulia upande mwingine, inaweza kuongeza ukubwa wa mgogoro na kuathiri zaidi watoto wanaohusika.
Mitandao si DNA
Kwa upande wake, mwanasheria wa masuala ya familia, wakili Anna Mrema, amesema migogoro ya ubaba wa mtoto ina taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa badala ya kufanywa mjadala wa mitandao ya kijamii.
Amesema pale ambapo kuna mashaka kuhusu ubaba wa mtoto, ushahidi wa kisayansi kupitia kipimo cha DNA unaweza kusaidia kupata majibu yenye msingi wa kisheria badala ya kulalamika kwa umma.
"Mitandao ya kijamii haiwezi kuwa mahakama. Kauli za watu, hisia au idadi ya wanaounga mkono upande mmoja haziwezi kuchukua nafasi ya ushahidi. Endapo kuna mgogoro, njia sahihi ni kufuata taratibu zinazotambuliwa na sheria," amesema Anna.
Mwanasheria huyo anafafanua kuwa katika kila hatua ya kutatua migogoro hiyo, masilahi ya mtoto yanapaswa kuwekwa mbele kuliko ushindani wa wazazi.