Watoto wafariki dunia kwa kukosa hewa wakicheza kwenye gari

Muktasari:
Watoto wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 6 na 7 wamefariki dunia kwa kukosa hewa wakati wakicheza ndani ya gari katika Kitongoji cha Ng’ung’ula Kijiji cha Jomu kata ya Tinde Wilaya ya Shinyanga.
Shinyanga. Watoto wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 6 na 7 wamefariki dunia kwa kukosa hewa wakati wakicheza ndani ya gari katika Kitongoji cha Ng’ung’ula Kijiji cha Jomu kata ya Tinde Wilaya ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Jomu, Juma Warioba na Diwani wa kata ya Tinde, Japhar Kanolo wamesema tukio hilo limetokea Agosti 22, 2023 saa 12 jioni wakati watoto wakicheza ndani ya gari ambalo lilijifunga, wazazi wao bila kujua kinachoendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai wazazi wa watoto hao walitokea Mwanza kwenda kusalimia nyumbani kwao Tinde.
“Jeshi la polisi tumepokea taarifa hizi, wazazi walitoka Mwanza wakiwa na gari lao kwenda kusalimia nyumbani kwao Tinde, walipofika pale hawakufunga milango ya ile gari na vioo vilikuwa vimefungwa hivyo gari lilijifunga na watoto kukosa hewa,
“Baada ya wazazi kushuka watoto walirudi kwenye lile gari wakaanza kuchezea likajifunga, kwa mujibu wa Daktari watoto wale walifariki kwa kukosa hewa”,ameeleza Magomi
Magomi amewataka wazazi kuwa waangalifu kwa watoto, pindi wanaposhuka kwenye magari wahakikishe wameyafunga ili kuepusha vifo visivyo vya lazima kama hivyo vilivyotokea.