Watoto 20 watajwa kubakwa, kulawiti ndani ya siku 60 Mara

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Majage Tandasi akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani la Manispaa hiyo leo Juni 10, 2024. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Vitendo hivyo vya ukatili vinadaiwa kuongezeka siku hadi siku, huku moja ya sababu ikidaiwa ni ugumu wa maisha pamoja na mifarakano ya ndoa.
Musoma. Zaidi ya watoto 20 wenye umri chini ya miaka 18 katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, wametajwa kubakwa na kulawitiwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Vitendo hivyo vya ukatili vinadaiwa kuongezeka siku hadi siku, huku moja ya sababu ikidaiwa kuwa ni ugumu wa maisha pamoja na mifarakano ya ndoa miongoni mwa wazazi.
Akitoa taarifa maalumu kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo leo Jumatatu Juni 10, 2024, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Majage Tandasi amesema migogoro ya ndoa pamoja na malezi ya upande mmoja, ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.
"Zipo sababu nyingi zinazosababisha ongezeko la vitendo hivi katika jamii, sababu hizo ni pamoja na ongezeko la watoto waliokosa uangalizi wa wazazi, hivyo kujilea wenyewe sambamba na uwepo wa kumbi za starehe zinazoruhusu watoto kuingia nyakati za usiku,” amesema Tandasi.
Pia amesema sababu nyingini ni wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule pamoja na kukosekana chakula cha mchana, husababisha watoto wanaotoka familia duni kupata vishawishi na kuingia kwenye uhusiano na watu wazima.
Hata hivyo, Tandasi amesema idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuwa baadhi ya matukio hayatolewi taarifa kutokana na ukosefu wa elimu kwa jamii.
“Matukio mengine hutolewa taarifa kwa kuchelewa, hivyo kusababisha kukosekana kwa ushahidi,” amesema.
Amesema ili kutokomeza vitendo hivyo, ni muhimu kutoa elimu kwa jamii kutambua madhara ya ukatili na namna ya kushirikiana na na vyombo vya dola pamoja na wadau.
Kutokana na taarifa hiyo, baraza hilo limeviomba vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Musoma kuweka mikakati ya haraka kutokomeza vitendo hivyo, huku likiitaka jamii kutimiza wajibu katika malezi na makuzi ya watoto.
"Huu ni msiba mkubwa, turudi katika utamaduni wetu, imefika mahali tunaiga mambo ya ajabu na ya aibu. Hebu turudi katika misingi yetu ya kiafrika, tupambane na haya mambo kwa vitendo,” amesema Asha Mohamed, Diwani wa Viti Maalumu.
Naye Mato Kuboja, Diwani wa Mwisenge amehoji kwanini watoto wanaruhusiwa kuingia kwenye kumbi za starehe wakati sheria na taratibu haziruhusu.
“Hii nayo ni hoja au changamoto kweli ya kuja kumwambia mtu? Lazima tukubaliane hizi ni stori kwa sababu kuna ugumu gani kusimamia sheria, kanuni na taratibu?” amehoji diwani huyo.
Akizungumza katika baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema bado kuna changamoto kubwa ya ukatili wa kingono kwa watoto, licha ya kuanza kutafutiwa ufumbuzi.
"Ni kweli tuna tatizo kubwa kwenye mji wetu wa Musoma na kwenye kikao chetu cha jana cha kamati ya ulinzi na usalama, tuliazimia tuanze kufanya makongamano ili watu waelewe ubaya wa haya mambo. Pia viongozi wa dini washirikishwe, kwa ujumla mapendekezo ni mengi na mazuri yote yatafanyiwa kazi," amesema.
Hata hivyo, amesema wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya jitihada ya kumaliza suala hilo, kuna umuhimu kwa jamii kuunga mkono vita hiyo.
“Wazazi wameacha majukumu yao, watoto wetu hawako salama, hivyo kila mtu anatakiwa kuhakikisha watoto wanakuwa salama," amesema Dk Haule.
Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase alisema watu 36 wamefikishwa mahakamani mwezi uliopita kwa tuhuma za ukatili wa kijinsia, ikiwemo ulawiti na ubakaji kwa watoto.
Morcase alisema kesi 13 zimetolewa hukumu ambapo watu watano wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja, huku wengine wakifungwa jela maisha na wengine adhabu mbalimbali.