Watoto 2,000 waondolewa mitaani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 12, 2023. Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni na Kamishina Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Baraka Kona. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Ni kupitia kampeni maalumu iliyoanza Agosti 2022 chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Dar es Salaam. Watoto 2,000 wameondolewa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kuunda kikosi kazi maalumu cha kuwaondoa mitaani na kuweka maofisa ustawi wa jamii katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mbezi Magufuli, Dar es Salaam na kile cha Nyegezi, mkoani Mwanza.
Agosti 2022 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilianza kampeni ya kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka wizara hiyo, Baraka Makona amesema hayo leo Jumanne, Desemba 12, 2023 katika kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) yanayotorajiwa kufanyika Desemba 18, mwaka huu.
Amesema katika utekelezaji wa kampeni ya kuwaondoa watoto mitaani walishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) na Jeshi la Polisi.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima amesema suala la watoto walio mitaani ni la jamii na hasa wazazi, hivyo wana jukumu la kuhakikisha hawarudi tena mtaani.
“Hili ni la jamii, anatoka nyumbani anaenda mtaani baba na mama hawamtafuti wala hawaripoti polisi, lakini anapotea ng'ombe au kuku mtaa mzima anatafutwa hawalali,” amesema.
Amesema watoto wanapoondoka majumbani huenda mtaani ambako hutumikishwa, hupitia ukatili wa kingono, kimwili na ukatili mwingine; mimba za utotoni na wengine husafirishwa.
“Natoa wito kwa wazazi, kama mtoto amekushinda mpeleke ustawi wa jamii, akitoroka mtafute mpeleke huko na kama mzazi una hali ngumu kuliko kumuacha aende mtaani kwa kudhani unapunguza tatizo unaliongeza. Mtaani atajifunza mabaya ambayo hutaweza kumrekebisha,” amesema.
Maadhimisho miaka 50
Akizungumza maadhimisho ya ustawi wa jamii, Dk Gwajima amesema yatafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Maadhimisho hayo yataambatana na usajili wa kulea watoto, kuwaasili, malezi ya kambo, usuluhishi wa migogoro ya ndoa, uchunguzi wa magonjwa ya macho, huduma kwa watu wenye ulemavu, vyeti vya kuzaliwa, ukatili na namna ya kukabiliana na ukatili,” amesema.
Dk Gwajima amesema maadhimisho hayo yanalenga kutangaza huduma za ustawi wa jamii na kuzifikisha karibu kwa umma.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imeahidi kuongeza nafasi za ajira 350 kwa maofisa ustawi wa jamii ili kupanua wigo wa upatikanaji huduma nchini.