Watoto 1,346 kutoka mtaani waunganishwa na familia zao
Muktasari:
- Watoto hao ni miongoni mwa 6,459 waliobainika wakati wa utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku 816 wakiunganishwa na mafunzo ya stadi za maisha na kupatiwa mitaji pamoja na vifaa vya kazi.
Dodoma. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Makundi Maalumu imewaunganisha na familia zao watoto 1,346 nchini waliokuwa wakiishi mitaani, katika kipindi cha kati ya Julai, 2021 hadi Aprili, 2024.
Watoto hao ni miongoni mwa 6,459 waliobainika wakati wa utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku 816 wakiunganishwa na mafunzo ya stadi za maisha na kupatiwa mitaji pamoja na vifaa vya kazi.
Watoto wengine 3,427 walipewa vifaa vya shule na mahitaji mbalimbali, 273 walipatiwa huduma ya kuimarisha uchumi wa kata huku 597 wakiendelea kupatiwa huduma kwenye vituo maalumu na makao ya watoto wakiandaliwa kwa ajili ya utengamano.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, imemnukuu waziri mwente dhamana Dorothy Gwajima akisema mikoa sita ilionekana kuwa na idadi kubwa ya kundi hilo ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Iringa na Dodoma.
“Baadhi ya athari za watoto kuendelea kuwepo mitaani ni kukosa malezi ya kiroho, elimu, matunzo ya afya ya mwili, kufanyiwa vitendo vya ukatili, kuingizwa kwenye kutumia ya dawa za kulevya na kuathirika na madhara yake,” amesema.
Ametaja madhara mengine ni baadhi yao kujihusisha au kutumiwa kwenye vitendo vya kihalifu hivyo ulinzi na usalama wa wananchi kuwa mashakani.
Wahamia maeneo mengine
Mkazi wa jiji la Dodoma, Peter Olomi amesema watoto wa mitaani bado wapo katika maeneo ya pembezoni mwa jiji ambapo wamekuwa wakiomba chakula, nauli na wakati mwingine wanakaa maeneo ambayo magari yanasimama.
“Unaweza usiwaone katika maeneo ya katikati ya jiji lakini hawa wapo wengi tu wamehamia katika maeneo ya pembezoni,” amesema.
Hata hivyo, Olomi amesema watoto wa kike wamepungua kwa kiasi kikubwa mitaani kuliko wa kiume.
Amesema wengi wa watoto hao hivi sasa wanatoka mikoa mingine ya kanda ziwa kama Mwanza, Shinyanga baada ya kuelezwa na wenzao kuwa Dodoma wanaweza kupata fedha.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Uhindini jijini Dodoma, Alnoor Kassam amesema katika mtaa wake hivi sasa hawaonekani baada ya kuwachukua na kuwapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto.
Amesema yeye mwenyewe aliwahi kuwaondoa watoto watatu mtaani na kuwarudisha shule ambapo wanaendelea vizuri na masomo.
“Ukitazama ni wazazi baada ya kuzaliwa baba hayupo, kamwachia mama, naye dawa za kulevya anajidunga. Mara nyingi hii inatokana na familia, watoto wanahangaika huko baada ya kuambiwa waende kutafuta chakula, sasa wakatafute wapi,” amesema.
Ameshauri suala la watu kufunga ndoa liangaliwe kwa makini kwa sababu wengi wa watoto wanaonekana kukimbilia mitaani, baada ya wazazi kufarakana na kusahau kama wana watoto wadogo.
“Tunataka hizi ndoa zitizamwe vizuri pande zote mbili kwa sababu kwa sasa yale mazingira kama ya zamani hayapo,” amesema Kassam ambaye mtaa wake ulikuwa ukikabiliwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani.
Amesema baada ya kuondoka mtaani kwa watoto hao hali imetulia hakuna vurugu tena.
Madhila yanayowakumba
Januari mwaka juzi, mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi 16, aliuawa kwa kuchomwa kisu shingoni wakati wakigombea gundi na mwenzake.
Ugomvi huo uliwahusisha watoto wa mtaani ambao walidaiwa kuwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya gundi katika eneo la Nyerere Square jijini Dodoma.
Februari mwaka jana, watoto sita wenye umri wa kati ya miaka 12 na 16 walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita wakisafiri chini ya basi kutoka mjini Bukoba mkoani Kagera kwenda jijini Mwanza.
Watoto hao wanaodai kuishi kwenye kituo cha mabasi Bukoba wamedai walililazimika kusafiri katika hali hiyo ili kufika Mwanza, ambako wanadhani kuna unafuu wa maisha ikilinganishwa na Bukoba.
Watoto hao waliingia kwenye basi la Happy Nation saa 9.00 usiku na kujificha kwenye ‘chassis’ ya gari hadi asubuhi lilipoanza safari ya kwenda Mwanza.
Watoto hao walidai kuwa kuna mwenzao aliwahi kupanda chini ya gari kutoka Bukoba hadi Mwanza na hakupata shida, akawaambia kuwa huko maisha ni mazuri na ndio maana waliamua kufanya hivyo.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Idara ya Ustawi wa Jamii unaonyesha kuwa watoto wa mitaani wamepungua kwa asilimia 27 mwaka 2020/2021 ikilinganishwa na mwaka 2017/2018.
Utafiti huo ulifanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Iringa na ulibaini uwepo wa watoto 6,393 mwaka 2018/2019 huku mwaka 2020/2021 ukibainisha uwepo wa watoto 4,383.
Katika kutambua na kutafuta suluhu, Aprili 12 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, ambapo mashirika mbalimbali huadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu.