Watatu waongezwa kesi ya jengo lililoporomoka Kariakoo

Muktasari:
- Itakumbukwa Novemba 29, 2024, wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo, ambao ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala, walifikishwa mahakama hapo na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wengine watatu wa Kariakoo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya 31 ya kuua bila kukusudia.
Wafanyabiashara hao ni Soster Nziku (55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe (59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku (28) mkazi wa Mbezi Beach.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Machi 26, 2025 na kusomewa shtaka la kuua bila kukusudia na kisha kuunganishwa na wenzao watatu wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Mshtakiwa Aloyce Sangawe anayekabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia akishuka ngazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Itakumbukwa Novemba 29, 2024, wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo, ambao ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala, walifikishwa mahakama hapo na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.
Hata hivyo, leo washtakiwa hao wapya, wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Roida Mwakambele mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Kabla ya kuwasomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulifanya mabadiliko katika hati ya mashtaka kwa kuwaongeza washtakiwa hao chini ya kifungu 234 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili Mwakamele aliyedai kuwa watu hao wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mwakamele ameiambia mahakama kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia namba 33633 ya mwaka 2024.
Amedai kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo uliopo eneo la Kariakoo isivyo halali, walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Mshtakiwa Soster Nziku akishuka ngazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya kuua bila kukusudia. Picha na Hadija Jumanne
Katika shtaka la pili mpaka la 31, wanadaiwa kusabisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.
“Wanadaiwa pia kusababisha kifo cha Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma,” amedai wakili huyo.
Amedai pia, wote kwa pamoja wanadaiwa kushindwa kutimiza majukumu yao na kusabisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, waliomba mahakama iwapatie dhamana kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika chini ya Kifungu namba 248 (1)(2) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mshtakiwa Stephen Nziku, akishuka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka yao ya kuua bila kukusudia.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba, hauna pingamizi juu ya dhamana kwa washtakiwa.
Hakimu Mhini alitoa masharti manne ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa au barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake kama ni waajiriwa.
Pia, amewataka kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja na wadhamini wao wawe wakazi wa jiji la Dar es Salaam na si vinginevyo.
Sharti lingine la dhamana wanatakiwa wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida).
Washtakiwa wote wametimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Mhini ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10, 2025.