Watanzania wapewa mbinu usalama wa chakula

Muktasari:
- Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya usalama wa chakula duniani, wataalamu wa lishe akiwemo Ofisa Lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Pendo Yaled amesema usalama wa chakula lazima uanzie shambani.
Iringa. Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Pendo Yeled amesema usalama wa chakula lazima uanzie shambani tangu wakati mazao yanapandwa, kuhudumiwa, kuvunwa, kusindikwa, kuhifadhiwa mpaka mezani.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) mtu mmoja kati ya 10 hupoteza maisha kila mwaka kwa kula chakula kichafu na kisicho salama.
Kulingana na takwimu hizo, watu 600,000 huugua kwa kula chakula hicho na 420,000 kati yao hufariki huku waathirika wakuu wakiwa ni wanawake wajawazito, watoto, wazee na watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 7, 2023 ofisini kwake, Yeled amesema hakuna njia nyingine ya kuhakikisha usalama wa chakula zaidi ya kuwa makini kwenye maandalizi yake tangu shambani mpaka kinafika mezani.
Amesema usalama wa chakula ni muhimu kwa maisha ya wanadamu kwa sababu tofauti na hapo ni hatari.
“Kama umevuna mahindi yako lazima uchambue, utoe mahindi yale yenye kuvu kuepuka sumu kuvu, tunashauri vyakula vingi vihifadhiwe kwenye mifuko inaitwa kinga njaa ili kisiharibike mapema mfano, mahindi,” amesema Yeled.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Gerad Mwamihamila amesema chakula salama ni kile ambacho mwanadamu akitumia kinamuwezesha kuishi.
“Kwenye eneo la uzalishaji lazima tuzingatie maeneo makuu ya maandalizi ya chakula hasa kwenye mbegu, maandalizi ya shamba mpaka hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kusindika,’ amesema Mwamihila na kuongeza; “Chakula kisicho na madhara kwa mwanadamu ni chakula salama.”
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Lishe, Matrida Erick ametaja maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa chakula usafi wa mazingira ya kuandalia chakula na vyombo, kupika kwa kina, kuhifadhi kwenye joto linalotakiwa au baridi na kuosha kwa maji safi kabla ya maandalizi mfano matunda na mboga