Watanzania waondoka na minoti ya Tap Kibingwa

Muktasari:
- Kampeni ya Tap Kibingwa, imelenga kuhamasisha matumizi ya miamala ya kidijitali kupitia Visa Debit Card.
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Visa imehitimisha kampeni yake ya “Tap Kibingwa” kwa droo ya mwisho iliyofanyika jijini Dar es Salaam, huku washindi watano wakitangazwa na mshindi wa gari jipya aina ya Suzuki Fronx akisubiriwa kutangazwa hivi karibuni.
Katika droo hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Coles Josette, Irene Charles Isaka, Chisora Kennedy, Abubakar Said Salim Bakhresa na Pietro Stella walitangazwa washindi wa zawadi ya Sh500,000 kila mmoja. Hii inafanya jumla ya washindi wa kampeni hiyo kufikia 15 waliopokea zawadi zenye thamani ya Sh7.5 milioni.
Akizungumza wakati wa droo hiyo, Meneja wa Kadi za Malipo wa Stanbic, Irene Mutahibirwa alisema kampeni hiyo imelenga kuhamasisha matumizi ya miamala ya kidijitali kupitia Visa Debit Card huku ikiwazawadia wateja waliotumia kadi hizo kwa uaminifu na kwa kiwango kikubwa.
“Tumefunga droo za kila mwezi kwa mafanikio makubwa, na sasa tunasubiri kwa hamu kumtangaza mshindi wa gari jipya ambaye atakuwa ni kilele cha kampeni hii,” alisema Irene.
Kampeni hiyo iliwahusisha wateja waliotumia angalau Sh2 milioni kwa mwezi, ambapo waliingia kwenye droo ya kila mwezi ya zawadi za pesa taslimu, huku wale waliotumia Sh5 milioni au zaidi wakijumuishwa pia kwenye droo kuu ya gari.
Mbali na zawadi, kampeni ya Tap Kibingwa imeelezwa kuwa jukwaa la kuongeza uelewa wa kifedha na kuhimiza matumizi ya huduma za kibenki za kidijitali, jambo lililosaidia kuongeza usalama na urahisi wa kufanya miamala.
“Tumeshuhudia jinsi wateja wetu walivyokumbatia teknolojia na huduma za kibenki mtandaoni kwa namna bora,” aliongeza Irene, akisisitiza dhamira ya benki hiyo kuendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na mahitaji ya soko.
Benki ya Stanbic imeahidi kuendeleza kasi hiyo ya ubunifu kwa kuleta bidhaa na huduma zaidi zinazomgusa mteja moja kwa moja, huku ikiendelea kuwa kinara wa ubunifu katika sekta ya kifedha nchini.