Matrilioni ya shilingi yanapita kwenye simu

Muktasari:
- Ripoti ya Mwaka ya Mwenendo wa Mifumo ya Malipo nchini kwa mwaka 2024 ya BoT inaeleza kuwa thamani ya malipo ya huduma kupitia simu za mkononi imefikia Sh198.85 trilioni katika mwaka 2024 kutoka Sh154.7 trilioni katika mwaka uliotangulia huku idadi ya mawakala ilifikia 1,475,281 mwaka 2024 kutoka 1,240,052, mtawaliwa.
Dar es Salaam. Uboreshaji wa huduma za mtandao, kukua kwa ujumuishaji kifedha, kupungua kwa matumizi ya fedha taslimu na upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kirahisi vimetajwa kuwa sababu za ongezeko la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu.
Sababu hizo zinatajwa na Benki kuu ya Tanzania (BoT) wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa thamani ya malipo ya huduma kupitia simu za mkononi imefikia Sh198.85 trilioni katika mwaka 2024 kutoka Sh154.7 trilioni katika mwaka uliotangulia.
Ukuaji huu unachochewa na ongezeko la miamala iliyofanywa sambamba na ongezeko la mawakala ya utoaji huduma za kifedha lililoshuhudiwa katika kipindi husika.
Ripoti ya Mwaka ya Mwenendo wa Mifumo ya Malipo nchini kwa mwaka 2024 ya BoT inaeleza kuwa, idadi ya mwaka ilifikia 1,475,281 mwaka 2024 kutoka 1,240,052 mwaka uliotangulia huku miamala ikifikia bilioni 6.413 kutoka bilioni 5.061, mtawaliwa.
“Ongezeko hili linachangiwa na ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa mawakala, ubunifu katika utoaji huduma na udhibiti unaofanyika. Mtandao mkubwa wa mawakala ulirahisisha ufanyaji wa miamala hata katika maeneo ya mbali,” inaeleza ripoti hii.
Pia BoT inaeleza kuwa kuwapo kwa sera za udhibiti zinazounga mkono matumizi ya huduma za kifedha kwa njia za simu ziliongeza imani ya watumiaji na kuongeza kiwango chao cha matumizi.
“Kuongezeka kwa matumizi haya pia kunadhihirisha hatua zinazolenga kuendeleza mazingira yanayounga mkono malipo ya kidijitali, kuboresha upatikanaji na ufikiaji huduma za kifedha huku ikichochewa na ufanisi na gharama nafuu,” imeeleza ripoti hiyo.
Mfano mzuri ni uvumbuzi kama vile Mfumo wa Malipo wa Haraka wa Tanzania (TIPS), ambao umeleta mapinduzi katika huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kuwezesha uhamishaji wa fedha baina ya mitandao kwa urahisi, kupunguza gharama za miamala na kuongeza matumizi na kupokelewa kwa huduma hii.
Wasemavyo wachumi
Mtaalamu wa uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi amesema matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yanarahisisha upatikanaji huduma na kupunguza gharama za ufanyaji wa biashara.
“Watu wanapofanya miamala kwa urahisi ni kitu ambacho kinakimbiza uchumi na kuongeza ufanisi, badala ya mtu kutumia saa mbili kutafuta tawi la benki na kutumia nauli anatumia sekunde chache kufanya miamala, inaokoa muda, matumizi ya fedha na kuongeza ufanisi kwa watu kazini,” amesema Dk Olomi.
Anasema njia rasmi za huduma za kifedha zinapotumia inaweka fedha kwenye mzunguko jambo ambalo inaleta tija zaidi kiuchumi tofauti na fedha hizo zingekaa nyumbani.
Mtaalamu wa Uchumi wa chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Lutengano Mwinuka anasema mzunguko wa kifedha katika uchumi unamaana kubwa na unapoongeza inamaanisha kuwa inaokoa muda waliokuwa wakiutumia kutafuta huduma.
“Mzunguko huu unamanisha kuwa kuna mapato yanaongezeka kwa serikali kutokana na tozo mbalimbali wanazopata hii inaifanya kupata fedha ambazo inaweza kutumia katika utekelezaji wa baadhi ya huduma za kijamii,” anasema Dk Mwinuka.
Anasema kuwapo kwa mzunguko huu pia unapunguza muda watu ambao walikuwa wakiutumia kusubiri fedha kutoka sehemu nyingine kwani wanakuwa na uhakika wa kuipata papo kwa pao jambo ambalo linafanya shughuli za kiuchumi kufanyika kwa kasi zaidi.
Miamala iliyofanywa
Mbali na walichokisema wachumi, Benki kuu inaelezea huduma hizi za kifedha kupitia simu za mkononi kupitia makundi tofauti ikiwemo ile inayofanywa kati ya mtu na mtu, mtu kulipia biashara na huduma, mtu kutuma fedha kutoka simu ya mkononi kwenda benki.
Uchambuzi unaonyesha kuwa, mwaka 2024, miamala ya mtu kwa mtu iliongezeka hadi kufikia milioni 479.11 yenye thamani ya Sh15.702 trilioni ikilinganishwa na miamala milioni 364.36 yenye thamani ya Sh11.323 trilioni iliyokuwapo mwaka uliotangulia.
Malipo kwa Biashara (P2B) pia ukuaji wake ulishuhudiwa kuanzia mwaka 2020, ambapo idadi ya miamala iliongezeka kwa asilimia 28.52 na thamani ya miamala ilikua kwa asilimia 45.76 mwaka 2024.
Jumla ya miamala ya malipo ya huduma na bidhaa bilioni 1.74 yenye thamani ya Sh26.602 trilioni ilishuhudiwa mwaka 2024.
Ongezeko hili kwa mujibu wa Benki kuu ya Tanzania linaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wafanyabiashara na kuashiria mabadiliko makubwa kuelekea miamala ya biashara yenye ufanisi zaidi na inayopatikana kwa urahisi.
“Ongezeko hili limechochewa na uvumbuzi wa ulipaji kwa kutumia simu kwa wafanyabiashara, unaojulikana kama LIPA Namba, miundombinu bora ya malipo, ukuaji chanya wa uchumi, mazingira ya udhibiti yanayounga mkono na leseni kwa watoa huduma wengi wa malipo,” imesema BoT.
Kwa upande wa kutoa fedha katika simu kwenda benki ambayo ni ishara ya utunzaji wa akiba miamala ilikuwa milioni 9.50 yenye thamani ya Sh3.6 trilioni mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.32 na asilimia 32.70, mtawalia.
Katika upande wakuhamisha fedha kutoka benki kwenda simu za mkononi miamala milioni 82.68 ya Sh11.29 trilioni ikiwa ni ukuaji wa asilimia 39.88 na asilimia 41.89, mtawalia.