Watanzania waitwa kupanda miti Mlima Kilimanjaro kuokoa barafu

Muktasari:
- Ili kupunguza makali ya kuongezeka kwa joto litokanalo na mabadiliko ya tabianchi, wadau wa mazingira wameamua kuja na kampeni ya kupanda miti Mlima Kilimanjaro ili kuikoa barafu iliyopo.
Dar es Salaam. Katika kuokoa mazingira ya Mlima Kilimanjaro ikiwemo barafu na miti, wadau wa mazingira kwa kushirikiana na Serikali wamewaita Watanzania kupanda miti takriban bilioni moja itakayosaidia kuokoa barafu iliyopo kwenye mlima huo.
Hatua hiyo inatokana na kuyeyuka haraka kwa barafu kwa sababu ya joto kali linalotokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoshuhudiwa duniani. Watafiti wanasema miaka 50 ijayo barafu iliyopo inaweza isionekane tena.
Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nessa iliyoandaa matembezi kuhamasisha upandaji huo wa miti, Deborah Nyakisinda amesema wamedhamiria hadi ifikapo mwaka 2050 wakamilishe idadi hiyo ya miti ingawa kwa sasa wanapanda miti milioni mbili kwa mwaka.
Amesema kampeni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2021 iitwayo ‘Save Mount Kilimanjaro’ imeandaa matembezi yatakayofanyika Mei 17, 2025 kuanzia geti la Marangu, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
“Tunaungana na Watanzania wote kwa pamoja ili kuokoa Mlima Kilimanjaro kwa kupanda miti kupitia matembezi haya ya kitaifa. Tutaanza na mikoa inayozunguka milima ya Manyara, Kilimanjaro, Arusha na Tanga ikiwa salama mikoa hii basi na barafu itakuwa salama.”
Akitaja umuhimu wa barafu ya mlima huo amesema ni chanzo cha maji, hewa nzuri iliyopo, chanzo cha watalii ambao kwa sasa wamefikia 65,000 kwa mwaka. Wanaokula na kulala kwenye hoteli za Kitanzania kuongeza mzunguko wa fedha na uchumi.
Amesema kuna kila sababu ya kutunza barafu hiyo kwakuwa ni muhimu kiuchumi na kijamii.
“Kwa upande wetu hatuwezi wenyewe tunaomba ushirikiano na wadau wengine tupate mingi zaidi, tuipande tuitunze ikuwe tuweze kufikia malengo. Kwa miaka mitano tunataka kupanda miti milioni 10 kwanza na kila mkoa upande walau 500,000.
“Tunataka tuilinde barafu tupunguze makali ya kuongezeka kwa joto ndio maana tunaungana na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) tuweze kufikisha jambo hili,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi anayeratibu kazi za utalii kanda ya Kaskazini Tanapa, Haika Bayona amesema suala la msingi kuhifadhi mazingira kwa maeneo ya jirani na maeneo ya hifadhi.
Amesema miti ikipandwa itaokoa mazingira ya Mlima na faida yake itakuwa kuongeza wageni ambao wanaendelea kumiminika nchini.