Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watanzania tisa warejea kutoka Israel

Naibu Waziri, Stephen Byabato akiongea na  watanzania aliowapokea wakiwa wametoka nchini Israel baada ya kurejeshwa nchini na Serikali kufuatia  changamoto ya hali ya usalama nchini humo iliyotokana na mapigano yanayoendelea hadi sasa.

Muktasari:

  • Watanzania tisa wamerejea nchini leo ikiwa zimetimia siku nne tangu Serikali kuwataka wajiandikishe ubalozini ili warejee nyumbani kufuatia mapigano yanayoendelea baina ya Israel na kundi la Hamas.

Dar es Salaam. Watanzania tisa waliokuwa Israel wamerejea nchini leo Oktoba 18, 2023 ikiwa zimetimia siku nne tangu Serikali kuwataka wajiandikishe ubalozini ili warejee nyumbani kufuatia mapigano makali yanayoendelea nchini humo.

Kurejea kwa Watanzania hao kumekuja baada ya kuzorota kwa usalama nchini humo kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Hamas kutoka Palestina ambapo hadi sasa maelfu wameshauawa na makumi elfu wamejeruhiwa.

Akizungumza baada ya kuwapokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Stephen Byabato amesema kurejea kwao kunatokana na utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kuwarejesha raia wake walioko nchini Israel ili waendelee kuwa salama.

"Serikali kupitia Ubalozi wake wa nchini Israel iliweka utaratibu wa kuwarejesha Watanzania wote ambao wangetaka kurudi nyumbani, niwahakikishieni kuwa Serikali itaendelea kuwashawishi walioko nchini humo ili waone haja ya kurudi nyumbani hadi pale hali itakapotengemaa ili waendelee kuwa salama.

Serikali imefarijika mno kwa Watanzania nyie kuitikia wito wa kuokoa maisha yenu, naanamini kuwa Watanzania wengine waliobaki nchini humo busara zao zitawaongoza na kuamua kurejea nyumbani ili waendelee kuwa salama, niwahakikishie kuwa Serikali itawarejesha nyumbani wote watakapokuwa tayari kufanya hivyo, wawe wawili au mmoja au 50 au 200, tuliweka utaratibu lakini nyie ndio mliojitokeza kwahiyo tukaamua tuanze na nyie," amesema Byabato

Akizungumza baada ya kupokelewa mmoja wa Watanzania hao Lucas Malaki ameishukuru Serikali kwa kitendo cha kuwarejesha nyumbani na kusema kuwa kitendo hicho kimewafanya wajisikie fahari kuwa watanzania na kuwaondolea unyonge na kuongeza kuwa wanakichukulia kitendo hicho kuwa ni cha upendo na cha kizalendo na kuahidi kuwa wataendelea kuwa raia wema.

Mtanzania mwingine Antony Mwaipopo amesema, "ningependa kuishukuru Serikali kwa dhati kabisa ya moyo wangu, kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kitendo hiki cha kutuwezesha kurejea nyumbani salama,”

Siku chache nyuma Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua aliliambia Mwananchi kuwa kuna zaidi ya Watanzania 350 waishio nchini humo huku wengi wao wakiwa ni wanafunzi.