Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubalozi Israel waendelea kusajili Watanzania watakaorudi nchini

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kutangaza mpango wa kuwarejesha nyumbani Watanzania waliopo nchini Israel, Ubalozi wa Tanzania nchini humo umesema mpaka jana mchana kazi ya kuwasajili ilikuwa inaendelea.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumapili Oktoba 15, 2023, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua amesema wanaendelea kuwasajili ingawa hana takwimu kamili za walioandikishwa mpaka alipokuwa akizungumza na Mwananchi jana, saa 8 mchana.

“Zoezi la kuwasajili walioamua kurudi nyumbani linaendelea, hivyo kwa sasa sina takwimu kamili,” alisema Kallua.

Juzi Jumamosi Oktoba 14, 2023, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa ya kuwataka Watanzania waliopo nchini humo kujiandikisha katika ubalozi wa Tanzania uliopo mjini Tel Aviv ili kurejeshwa nchini.

“Kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini Israel na maeneo mengine ya jirani, Serikali imeandaa mpango wa kuwarejesha nchini Watanzania waliopo nchini humo,” ilieleza taarifa hiyo ya wizara.

Hii si mara ya kwanza Watanzania kurejeshwa nyumbani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama katika mataifa waliyopo, kwani walishawahi kurejeshwa kutoka Sudan na Ukraine ambako kuna mapigano yanayoendelea hadi sasa.

Hatua hiyo inatokana na mapigano yaliyozuka Jumamosi iliyopita, baada ya wanamgambo wa Hamas kutoka Palestina kurusha makombora nchini humo na baadaye Serikali ya nchi hiyo kupitia waziri wake mkuu, Benjamin Netanyahu kutangaza vita. Mpaka sasa maelfu ya watu wameuawa na wengine kujeruhiwa.

Mbali na Tanzania, Ugiriki pia limewahamisha raia wake takribani 90 waliokuwa wamekwama Israel kutokana na mapigano katika nchi hiyo.

Pia tovuti ya Bmeia imesema raia 162 wa Austria wamehamishwa kutoka Israeli hadi Vienna, miongoni mwao walikuwa Waaustria 81 pamoja na wanafamilia wasio Waaustria pamoja na raia kutoka mataifa mengine 14 wakiwemo watoto 12.




Majeruhi, vifo vyapaa

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, idadi ya vifo Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi ilifikia Wapalestina 2,383 huku 10,814 kujeruhiwa hadi jana asubuhi, kulingana na vyanzo vya Wizara ya Afya ya Palestina.

Wakati huohuo, Shirika la Anadolu Agency limesema idadi ya vifo Israeli hadi sasa ni 1,300 na idadi ya Waisraeli waliothibitishwa kujeruhiwa inazidi 3,400.


Guteres azidi kulia na Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito kwa Israel kuepusha 'janga la kibinadamu'.

Guterres amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na viongozi Israeli akiwahimiza kuepusha janga hilo. Pia amekuwa akiwasiliana na mabalozi mjini New York na maofisa wengine wakuu katika Mashariki ya Kati.

Alisema ni muhimu kuwalinda raia wote, wakiwemo wale wanaohifadhiwa katika shule za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina (UNRWA) pamoja na ufikiaji wa kibinadamu kwa raia waliokwama ndani ya Ukanda wa Gaza ili kuzuia vifo zaidi.


WHO yaionya Israel

Wakati Guterres akisema hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema amri za Israel za kuwalazimisha kuhama kwa wagonjwa kaskazini mwa Gaza ni hukumu ya kifo kwa wagonjwa hao pamoja na waliojeruhiwa.

Kauli hiyo imekuja baada ya Israel kuwataka takriban raia milioni 1.1 kuondoka eneo la kaskazini mwa eneo hilo, kabla ya kile kinachotarajiwa kuwa hatua kubwa ya kuingia Gaza na vikosi vya ardhini vya Israel, ikikamilika.

Pia limelaani vikali maagizo ya mara kwa mara ya Israeli ya kuwataka wagonjwa kuhama katika hospitali 22 zinazohudumia zaidi ya wagonjwa 2,000 kaskazini mwa Gaza.

“Kuhamishwa kwa lazima kwa wagonjwa na wafanyakazi wa afya kutazidisha janga la sasa la kibinadamu na afya ya umma,” imeeleza taarifa iliyowekwa tovuti ya WHO.

WHO imesema maisha ya wagonjwa wengi mahututi na dhaifu ikiwemo wale walio katika uangalizi wa karibu au watoto wachanga katika incubators, wajawazito wenye matatizo na wengine wote wanakabiliwa na kuzorota kwa hali yao au kifo ikiwa watalazimika kuhama na kukatishwa kwa matibabu.

Vituo vya afya kaskazini mwa Gaza vinaendelea kupokea wimbi la wagonjwa waliojeruhiwa na vinafanya kazi zaidi ya uwezo wake, huku baadhi ya wagonjwa wakipatiwa matibabu katika korido na nje katika mitaa jirani kutokana na ukosefu wa vitanda hospitalini.

WHO inaitaka Israel kutengua mara moja maagizo ya kuhama kwa hospitali za kaskazini mwa Gaza na kutoa wito wa ulinzi wa vituo vya afya, wahudumu wa afya, wagonjwa na raia.

Pia inasisitiza kuwasilishwa haraka vifaa vya matibabu, mafuta, maji safi, chakula na misaada mingine ya kibinadamu hadi Gaza kupitia kivuko cha Rafah, ambapo msaada wa kuokoa maisha unaendelea.


Unicef yaeleza hali halisi ya watoto

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef), limesema maelfu ya watoto na familia zao wameanza kukimbia kaskazini mwa Gaza kabla ya mashambulizi makubwa yanayokaribia ya Israel.

Shirika hilo linasema takriban wiki moja baada ya vita hivyo, mamia ya watoto wameripotiwa kuuawa huku maelfu wakiripotiwa kujeruhiwa.

Unicef inataka kusitishwa kwa mapigano huku watu milioni 1.1 karibu nusu yao wakiwa watoto wamehama, kabla ya kile kinachotarajiwa kuwa shambulio kubwa la kijeshi katika moja ya maeneo yenye watu wengi zaidi duniani.

“Watoto na familia huko Gaza wamekosa chakula, maji, umeme, dawa na ufikiaji salama wa hospitali, kufuatia siku za uhasama na kukatwa kwa njia zote za usambazaji. Hali ni janga na mashambulizi ya mabomu yasiyokoma na ongezeko kubwa la uhamisho wa watoto na familia. Hakuna maeneo salama,”

Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Catherine Russell alisema kusitishwa kwa mapigano mara moja na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ni vipaumbele vya juu kuruhusu misaada inayohitajika kwa watoto na familia huko Gaza.

“... Watoto huko Gaza wanahitaji usaidizi wa kuokoa maisha na kila dakika ni muhimu,” alisema.

Taarifa ya Unicef imeongeza kuwa nyumba na miundombinu muhimu vimeharibika na zaidi ya watu 423,000 wamekimbia makazi yao. Baadhi wamejihifadhi katika shule au hospitali, huku baadhi ya shule zikiharibiwa kwa mashambulizi.

(Kwa msaada wa mtandao)