Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanne wafariki kwa shoti ya umeme msibani

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo limetokea leo Jumanne saa 3:40 asubuhi katika Mtaa wa Ngugwini

Handeni. Watu wanne wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati wakifunga maturubai msibani Mtaa wa Ngugwini, Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo limetokea leo Jumanne saa 3:40 asubuhi katika mtaa huo.

“Waliofariki dunia katika tukio hilo ni Fredy William Mwangunda (43), Mhina Athuman Mangagwa (35), Andrew Allen Mkomwa (29) na Salehe Omary Machaky (25) aidha, majeruhi ni William Gumbo (50) na Mbega Ally (49),” amesema Kamanda Mchunguzi.

Mkazi wa Handeni Omari, amesema watu walipumzika kwa ajili ya kusubiria shughuli ya mazishi, lakini ukatolewa utaratibu wa kutenga maturubai kuyasogeza upande mwingine.

Amesema vijana wanane walinyanyuka kwa ajili ya kuanza kuyatenganisha maturubai hayo na kunyanyua mahema bila kuangalia juu kulikokuwa na nyaya za umeme.

“Uliwekwa utaratibu wa turubai moja kusogezwa upande wa pili ili kupata nafasi zaidi, sasa waliokuwa wakifanya hivyo hawakuangalia juu na bahati mbaya waligusa nyaya za umeme na kupigwa shoti,” amesema Kibinda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Eilaya ya Handeni, Albert Msando amesema vijana wanane walihusika kwenye tukio hilo, hivyo wanne wamefariki dunia na wengine wapo hospitali.

Amesema amefika hospitali ya kukuta majeruhi wanaendelea vizuri na kuwataka wananchi kuwa na subra na wasihusishe na masuala mengine.

“Katika hili ndugu wote ambao mmekutwa na tukio hili, Serikali itagharamia shughuli za mazishi na kuwahudumia wale waliojeruhiwa na kama familia itahitaji msaada mnaweza kuwasiliana nasi kupitia viongozi waliopo hapa, hii ni ajali kama ajali nyingine tutashirikiana kuhakikisha tunawahifadhi ndugu zetu bila changamoto yoyote,”amesema Msando.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Handeni, Mussa Chowo amekiri watu hao wamegusa laini kubwa ya umeme, hivyo  wakapigwa na shoti.

Meneja huyo ameshauri wananchi kuendelea kuchukua tahadhali kufanya shughuli za kibinadamu chini ya miundombinu ya umeme, kwa kuwa kufanya hivyo ni hatari kwao.

Jumla ya watu 12 wamefariki dunia leo Desemba 24, 2024 wilayani humo baada ya wanne kupigwa shoti na wanane kupoteza maisha kwenye ajali ya gari.