Wanne kortini wakidaiwa kusafirisha kilo mbili za heroin, mirungi

Washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha kilo 2 za heroin na mirungi, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Januari 16, 2025 katika eneo la Survey na mtaa wa Ukombozi uliopo Kariakoo, ambapo walikutwa wakisafirisha kilo mbili za heroini na gramu 96 za mirungi.
Dar es Salaam. Wakazi wanne wa Jiji la Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo heroin zenye uzito wa kilo 2.44
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Abdallah Mwita (38) mkazi wa Magomeni, Abdallah Maggid (32) mkazi wa Survey, Said Alawy (40) mkazi wa Kariakoo na Halima Mwidini Nuru (23) mkazi wa Kariakoo.
Washtakiwa hao wamesomewa mashitaka yao jana jioni, Februari 28, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.
Kabla ya kusomewa mashitaka hayo, hakimu Kiswaga aliwaambia washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mashitaka yanayowakabili, Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Pia kiasi cha dawa walichoshtakiwa nacho mshtakiwa wa kwanza hadi wa watatu hakina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Baada ya hayo, walisomwa mashitaka yao ambapo wakili Mbilingi, ambaye alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5208 wa mwaka 2025.

Akiwasomea mashitaka yao, wakili Mbilingi alisema kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kusafisha dawa hizo kinyume kifungu cha 15A(1) na (2) C cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alidai shitaka la kwanza linawakabili Mwita, Maggid na Alawy, ni kusafirisha kilo mbili za heroini kinyume cha sheria.
Alidai Januari 16, 2025 eneo la Survey lililopo wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa Mwita, Maggid na Alawy walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 2.44, kinyume cha sheria.
Shtaka la pili ni kusafirisha mirungi, linalomkabili Alawy na Halima, ambapo wanadaiwa Januari 16, 2025 katika Mtaa wa Ukombozi uliopo eneo la Kariakoo, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha mirungi yenye uzito wa gramu 96.45.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashitaka yao, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Mbilingi alidai mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo ( Halima) shitaka linalomkabili lina dhaminika hivyo kuomba Mahakama itoe masharti ambayo yatamfanya mshtakiwa huyo kuhudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi yake inapotajwa.
Hakimu Kiswaga alisema atatoa masharti ya dhamana dhidi ya Halima, Machi 4, 2025.
Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Jumanne ya wiki ijayo na washtakiwa wamerudishwa rumande.