Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanne familia moja wafariki kwa kusombwa na mafuriko Arusha

Magari yakiwa kwenye foleni eneo la Kwa Msomali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro barabara ya Arusha kwenda Kilimanjaro wakisubiri maji yapungue barabarani kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumanne Aprili 25, 2023.

Muktasari:

  • Mvua kubwa iliyonyesha mkoani Arusha usiku wa kuamkia leo imeacha majonzi baada ya watu wanne kupoteza maisha baada ya gari waliyokuwa wamepanda kusombwa na mafuriko.

Arusha. Watu wanne wa familia moja wamefariki na wengine wawili wamelazwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa na mafuriko wakiwa safarini kwenda Kilimanjaro katika eneo la King'ori Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

 Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Jumanne Aprili 25, 2023 kutokana na mvua kubwa ambazo zimenyesha mkoani humo usiku wa kuamkia leo hadi majira ya alfajiri na kusababisha barabara kadhaa kufungwa.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Justin Masejo amethitisha tukio hilo leo jioni lililosababisha watu wanne kupoteza maisha baada gari yao kusombwa na maji wakiwa safarini kutoka Arusha kwenda Kilimanjaro na akaeleza uchunguzi bado unaendelea kutambua miili hiyo.

"Siwezi kusema ni watu wa familia moja ama la ila kama alivyosema Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (Emmanuela Kaganda) tukio hilo limetokea leo," amesema

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda akizungumza na waandishi wa habari amesema gari lililopata ajali lilikuwa linaendeshwa na Naimani Metiri ambaye amelazwa Hospitali ya Bona wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Katika ajali hiyo pia abiria mmoja ambaye ameokolewa, Angella Metiri (36) amelazwa katika hospitali hiyo kutokana na ajali hiyo.

Waliofariki ni Colin Lyimo (16) mwanafunzi Ilboru Sekondari, Lisa Mitiri (8), Brenda Amani (25) na Martha Metiri (40).

 "Ajali imetokea baada ya gari aina ya Noha iliyokuwa imebeba abiria watano kusombwa na maji ambapo watu wanne walibainika kufariki na wawili kuokolewa akiwepo dereva ambao bado wanapata huduma" amesema.

Kaganda amesema wilaya hiyo imepokea kwa huzuni tukio hilo ambapo ametoa pole kwa familia zilizo wapoteza wapendwa wao na kuwakumbusha wananchi kuenzi tamaduni za Watanzania pale linapotekea tatizo kusaidia badala ya kujikita kupiga picha

Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya ya Hai, Amir Mkalipa amesema mvua zinazoendela kunyesha katika wilaya hiyo imesababisha madhara makubwa ikiwemo huduma za usafirishaji kusimama kwa muda kutokana na mawasiliano ya barabara kukatika.

Amesema katika wilaya hiyo, mashamba mengi yenye mazao yalisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendela kunyesha katika maeneo mbalimbali ambapo alisema mpaka kufika mchana hali ilikuwa shwari na magari yaliweza kuendelea na safari zake.

"Katika wilaya ya Hai, kumetokea maafa yaliyosababishwa na mafuriko ambayo yamesbabaisha mafuriko katika kata ya Kia, maji yamekatisha kwenye mashamba ya wananchi na mimea midogo ya mahindi ambayo yako mashambani kuna sehemu yamepata adhari kwa kuzolewa na maji," amesema DC Mkalipa.
Naye, Kaimu Meneja Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Benitho Mdzovela, amesema kutokana na kuwepo changamoto ya mafuriko katika daraja la mto Biriri eneo la Kwa Msomali, wilayani Hai tayari wamewasiliana na Mtendaji Mkuu wa Tanroad kuona namna ya kuongeza ukubwa wa daraja hilo ili maji yasikatize tena barabara na kusababisha adha kwa vyombo vya usafiri.

"Leo tumepata changamoto ya mafuriko katika eneo la Kwa msomali eneo la daraja la mto Biriri, kumetokea mafuriko ambayo yameleta madhara katika barabara ya Moshi kwenda Arusha, ambapo daraja la mto Biriri lilikuwa limezidiwa maji na kupita juu ya barabara," amesema.

Machi 3 mwaka huu katika eneo hilo hilo kulitokea mafuriko makubwa na kusababisha adha ya usafiri ambapo mabasi yaendayo sehemu mbalimbali nchini yalishindwa kuendelea na safari zake kwa zaidi ya saa 3 hali ambayo ilisababisha usumbufu kwa abiria ikiwemo abiria kuchelewa kufika wanakoelekea kwa wakati.