Wanazuoni wataka ujuzi mtambuka kuingizwa kwenye mitalaa

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam, Dk Elizaberth Mwakasangula akizungumza katika kongamano lililohusisha wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali mkoani Morogoro. Picha na Lilian Lucas.
Muktasari:
- Wanazuoni wamependekeza kuingizwa kwa ujuzi mtambuka katika mitalaa ya elimu ili kuwawezesha wahitimu kujiamini.
Morogoro. Licha ya Serikali kuweka nguvu kwenye mitalaa inayotoa elimu ya ufundi, imeshauriwa kuingiza ujuzi mtambuka 'Soft Skills' kama nyenzo ya ujasiri kwa wahitimu wa vyuo katika kupata ajira.
Ushauri huo, umeambatanishwa ule wa kuitaka Serikali iwe inafanya maboresho ya mara kwa mara ya mitalaa ili kuendana na mabadiliko ya ulimwengu.
Hayo yameelezwa leo, Jumapili Novemba 5, 2023 na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Calvin Mwita alipozungumza katika kongamano la wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali mkoani Morogoro.
Amesema mitalaa hiyo itawawezesha wahitimu kuwa bora zaidi hasa nyakati za ajira.
“Tunapendekeza vyuo vikuu kuwa na mitalaa inayolenga kumsaidia mwanafunzi moja kwa moja na ujuzi wa ufundi pamoja na ujuzi mtambuka, sio abaki kuegemea zaidi kwenye upande wa ujuzi wa kiufundi," amesema.
Alitumia jukwa hilo, kueleza umuhimu wa mapitio ya mara kwa mara ya mitalaa, akidokeza unasaidia kuendana na mabadiliko ya ulimwengu.
Hata hivyo, hoja yake kuhusu ujuzi mtambuka imetokana na kile alichoeleza, ilifanyika utafiti uliobaini idadi chache ya wanafunzi wenye ujuzi huo.
"Wenye huu ujuzi ni wachache ambao wamekuwa wakijisomea vitabu na kuangalia video kupitia mitandao ya kijamii na wanajikuta wana uwezo wa kunieleza vizuri," amesema.
Amewataka wanafunzi wajiunge na taasisi zitakazowasaidia kuwa na ujuzi huo sambamba na kuhudhuria makongamano na semina zitakazowajenga kuwa na ujuzi mtambuka.
Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam, Dk Elizaberth Mwakasangula amesiaitiza umuhimu wa kuwa na ujuzi huo.
Aidha, amewasihi wanafunzi kutambua kwa kujifunza zaidi na kujua masuala ya ujuzi mtambuka kwa kujenga tabia ya kusikiliza wanayofundishwa, kusoma vitabu mbalimbali na kutumia mitandao ya kijamii kujifunza hasa suala la kujiamini.