Wanaosoma nje ya Tanzania masharti haya yanawahusu

Naibu Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga
Muktasari:
- Serikali imesema utaratibu ni lazima waombaji wa vyuo vya nje wapate barua za kuwatambulisha na kuwasaidia kupata vyuo na kozi wanazokwenda kusoma.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imetoa maelekezo na masharti kwa watu wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi ikiwamo kuwa na barua maalumu inayotolewa na Serikali ili kujua wanakwenda kusoma nini na katika chuo gani.
Maagizo hayo yametolewa leo Jumatano Aprili 23, 2025 na Naibu Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ng’wasi Kamani.
Mbunge huyo ameuliza upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha vijana wanaohitimu masomo nje ya nchi wakiwemo waliosoma katika nchi za Afrika Mashariki wanasajiliwa katika mifumo ya elimu nchini.
Mbunge huyo amesema kwa sasa vijana waliosoma nje ya nchi wapo mitaani wanahangaika, kwani wanakataliwa kusajiliwa na taasisi husika kwa madai ya kutokutambua elimu zao.
”Nitoe wito na ushauri kwa wale wanaotaka kwenda nje, wahakikishe wanapata cheti cha kutambua wanakwenda kusoma chuo gani na taaluma ipi, kuwalinda wao na taaluma zisiweze kuleta athari nje ya nchi,” amesema Kipanga.
Kipanga amesema vijana wanaotaka kwenda kusoma nje wanatakiwa kupewa hati ya ruhusa (cheti) kabla ya kwenda nje kusoma, Serikali itawezesha kutambua chuo na kozi anaporudi iweze kutambua na kumsajili kutokana na taaluma aliyopata.
Kuhusu Serikali kuwasaidia waliosoma Vyuo vya Afrika Mashariki, amesema usajili wa wahitimu kutoka vyuo vya nje ya nchi ikiwa ni pamoja na vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hufanywa na mamlaka za usajili au bodi za kitaaluma kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
Amesema kabla ya usajili muhitimu hutakiwa kupeleka vyeti vya taaluma Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na wale wa stashahada na cheti huvipeleka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kuvithibitisha, kufanya ulinganifu wa sifa na kiwango cha elimu. “Hivyo napenda kuwasihi wahitimu wote kutoka vyuo vya nje ya nchi kufuata utaratibu uliopo ili kupata usajili.