Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi walia tofauti za kisiasa kukwamisha ujenzi wa kituo cha afya

Baadhi ya viongozi wa kata ya Nankanga walioshiriki katika mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika wilaya ya Sumbawanga vijijini

Muktasari:

  • Waziri Sangu amewataka viongozi wa vijiji na kata kushirikiana bila kuzingatia tofauti za vyama vya siasa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rukwa. Wananchi wa Kata ya Nankanga, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, wamedai tofauti za kisiasa miongoni mwa baadhi ya viongozi wa vijiji na diwani wa kata hiyo zinachelewesha upatikanaji wa eneo la kujenga kituo cha afya, hali inayowaathiri wananchi wanaohitaji huduma za matibabu.

Wakizungumza leo, Jumatano, Julai 22, 2026, mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano wa Kazi, Deus Sangu, katika ziara yake ya kikazi mkoani Rukwa, wananchi hao wamesema kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya baadhi ya viongozi wa vijiji na Diwani wa Kata ya Nankanga, Emanuel Saasita Kishangu (NCCR-Mageuzi), kumekuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo muhimu.

Mmoja wa wananchi, Maria Nzumi, amesema ucheleweshaji wa ujenzi wa kituo cha afya unaendelea kuwaathiri zaidi wajawazito, watoto na wazee, ambao hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kata jirani.

"Kama ninyi viongozi mna changamoto zenu za kisiasa, ziwekeni pembeni. Linapokuja suala la maendeleo, leteni maendeleo badala ya kulumbana," amesema Nzumi.

Akizungumzia malalamiko hayo, Waziri Sangu amewataka viongozi wa vijiji na kata kushirikiana bila kuzingatia tofauti za vyama vya siasa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Sangu, ambaye pia ni mbunge wa Kwela, ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nankanga, Tarafa ya Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga.

Amesema viongozi wanapaswa kuiga mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameunda Serikali inayoshirikisha viongozi wenye itikadi tofauti za kisiasa kwa lengo la kuwatumikia wananchi.


"Tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo katika kutatua changamoto za wananchi. Maendeleo yanahitaji mshikamano na ushirikiano wa viongozi wote bila kujali vyama vyao," amesema Sangu.

Amesema hata katika wizara anayoiongoza, viongozi wenye mitazamo tofauti ya kisiasa wanafanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kutekeleza majukumu ya Serikali, akitolea mfano ushirikiano kati yake na Naibu Waziri, Dk Eveline Munisi.

"Mimi ni Waziri ninayeshughulikia kazi, ajira na uhusiano wa kazi. Tunafanya kazi kwa pamoja bila kuangalia tofauti za kisiasa kwa sababu lengo letu ni kulitumikia taifa na kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan," amesema.

Aidha, amesema wizara yake ina jukumu la kuratibu uhusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwamo vyama vya siasa, na kwamba hivi karibuni ilifanya kikao kazi na viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na maridhiano nchini.

Awali, Diwani wa Nankanga, Emanuel Saasita Kishangu, aliwasilisha changamoto zinazoikabili kata hiyo, ikiwamo ukosefu wa kituo cha afya, upungufu wa madawati na uchakavu wa miundombinu ya shule za msingi.

Baada ya kupokea taarifa hizo, Sangu amekabidhi madawati 20 yenye thamani ya Sh2 milioni kwa Shule ya Msingi Nankanga, pamoja na mifuko 100 ya saruji na mabati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Shule Shikizi ya Nankanga C.