Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi walalamikia katikakatika ya umeme, Tanesco wafafanua

Muktasari:

  • Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27 jana Aprili 1, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema kukatikatika kwa umeme kunapojitokeza hivi sasa, si upungufu wa nishati hiyo, bali uimarishaji wa gridi ya Taifa.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kwa sasa hakuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini, isipokuwa pale hitilafu zinapojitokeza kwa wateja mmoja mmoja.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamelalamikia hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na wakati mwingine kupungua kwa nguvu, jambo linalowaweka katika hofu ya kuharibika kwa vifaa vyao vinavyotumia nishati hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini humo, wakazi wa maeneo ya Kimara, Kibamba, Kinyerezi na Tabata Kimanga wamesema changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza hususan usiku.

Mkazi wa Kibamba, Shabani Omari amesema katika wiki za hivi karibuni umeme umekuwa ukikatika mara kadhaa, hasa usiku, hali inayotanguliwa na kupungua kwa nguvu ya umeme.

Amesema hali hiyo husababisha baadhi ya vifaa vya umeme kama friji, pasi na majiko ya umeme kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

“Kwa wiki mbili hizi hali hiyo imejitokeza zaidi ya mara tano, na inatia hofu ya kuunguliwa kwa vifaa vinavyotumia umeme,” amesema Omari.

Kwa upande wake, mkazi wa Kimara, Ashura Abdallah amesema kwa takribani siku tatu mfululizo kumekuwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara, hasa usiku.

Ameeleza kuwa wakati mwingine baadhi ya nyumba hupata umeme huku nyingine zikikosa huduma hiyo, na umeme unapokatika huchukua kati ya dakika 30 hadi saa moja kurejea.

“Kwa siku unaweza kukatika zaidi ya mara moja, hali ambayo inasumbua sana,” amesema.

Naye Mirfat Juma, mkazi wa Tabata Kimanga amesema hali hiyo hujitokeza zaidi ya mara tatu kwa wiki, huku umeme ukichukua muda wa dakika 30 hadi saa moja kurejea.

Ameongeza kuwa wakati mwingine Tanesco hutoa taarifa ya kukatika kwa umeme kwa ajili ya matengenezo, lakini muda wa kukatika huongezeka bila taarifa kwa wananchi.

“Mara nyingine wanatangaza muda wa kukatika, lakini huongeza muda bila kutoa taarifa ya ziada,” amesema.

Kwa upande wake, Sakina Ibrahim wa Kinyerezi amesema katika baadhi ya maeneo umeme umekuwa ukipatikana kwa baadhi ya nyumba huku nyingine zikikosa kabisa au kuwa na nguvu ndogo.

“Jana nyumba nne tu katika mtaa wetu zilikuwa na umeme, nyingine hazikuwa nao. Baada ya kuripoti, ilichukua takribani saa moja na nusu huduma kurejea,” amesema.

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Tanesco, Irene Gowelle amesema huduma ya umeme nchini ipo imara na inapatikana wakati wote, isipokuwa pale kunapotokea changamoto za kiufundi kwa wateja binafsi.

Amesema wateja wanaopata hitilafu wanapaswa kutoa taarifa katika vituo vya huduma kwa wateja ili waweze kuhudumiwa kwa haraka.

“Hakuna changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini. Huduma ipo vizuri na inapatikana wakati wote, isipokuwa changamoto ndogondogo kwa wateja mmoja mmoja ambazo hushughulikiwa kupitia vituo vya huduma kwa wateja,” amesema.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alisema kukatika kwa umeme kunakoshuhudiwa kwa sasa hakutokani na upungufu wa nishati hiyo, bali ni matokeo ya kazi ya kuimarisha gridi ya Taifa.

Amesema umeme ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kisasa, ukichangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za viwanda, teknolojia na matumizi ya nyumbani.

Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa umeme ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kupunguza changamoto ya kukatika katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kuunganisha wilaya ambazo bado hazijaunganishwa katika gridi ya Taifa.