Umeme wa uhakika wafungua milango ya uwekezaji Kilombero
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Daunstan Kyobya, amewakaribisha wawekezaji kuwekeza kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika baada ya kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme Ifakara kilichojengwa na REA. Kituo hicho kinazalisha megawati 18 huku mahitaji yakiwa saba, hivyo kuwepo ziada ya megawati 11.
Ifakara. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Daunstan Kyobya amewaomba wadau mbalimbali kuwekeza katika wilaya hiyo kwa kuwa kuna fursa nyingi kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika. Amesema hali hiyo imetokana na kukamilika kwa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme Ifakara kilichojengwa kwa ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Akizungumza leo Machi 31, 2026 wakati wa ziara ya kutembelea kituo hicho, mkuu huyo wa wilaya amesema kituo hicho kinachopokea umeme kutoka vituo vya kuzalisha umeme Kidatu na Kihansi, kinazalisha megawati 18 na zinazotumika katika wilaya ya Kilombero na Ulanga ni megawati saba pekee.
"Matumizi ya umeme kwa Kilombero na Ulanga ni megawati saba, hivyo kuna ziada ya megawati 11 ambazo hazitumiki kwa sasa. Wawekezaji waje kwa sababu sasa kero ya kukatika-katika kwa umeme imekwisha.
"Kuna fursa za uwekezaji kwenye uchimbaji madini, utalii kwenye hifadhi ya Nyerere, Udzungwa na kilimo cha ufuta, viungo, pamba, korosho, miwa na parachichi," amesema.
Awali, Meneja wa Usimamizi wa Miradi wa Rea, Mhandisi Deogratius Nagu amesema ujenzi wa kituo hicho umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa wilaya ya Kilombero na Ulanga kwa kufungua zaidi shughuli za kiuchumi.
"Gharama na ujenzi wq kituo hiki ni Sh25 bilioni ambazo zimetolewa na Serikali, hivyo kuondoankero ya umeme kukatika mara kwa mara ."amesema.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro Kusini, Masingita Lugati amesema kabla ya ujenzi wa kituo hicho, walikuwa wakitegemea laini moja ya umeme kutoka Kidatu ambayo ilikuwa ikitoka umbali wa kilomita 75 kwenda Mahenge na Malinyi, hali iliyochangia kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Muonekano wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara.
"Kutokana na umbali kilipo kituo, uhakika wa upatikanaji wa umeme ulikuwa mdogo, lakini sasa wananchi wameondokana na changamoto hiyo," amesema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile amesema uwekezaji unaofanywa na Rea unaliondoa Taifa katika unyonge uliokuwepo miaka ya nyuma.
"Zamani ulikuwa ukisafiri ukiona mwanga ulikuwa unajua umefika mjini, lakini hali hiyo sasa ipo kila sehemu. Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanyika," amesema.
Kauli za wanufaika
Miongoni mwa taasisi zilizonufaika na ujenzi wa kituo hicho ni Shule ya Sekondari Ifakara, na mkuu wa shule hiyo, Setina Ngailo amesema wanafunzi hawajawahi kulala gizani, na wanapata muda zaidi wa kujifunza, hivyo kuongeza ufaulu.
Amesema pia uwepo wa umeme wa uhakika umesaidia upatikanaji wa maji muda wote.
Kwa upande wa wafanyabiashara, msimamizi wa kiwanda cha kukoboa mpunga cha Buzelengule, Enos Machimu amesema uwepo wa umeme wa uhakika umewaongezea wateja.
"Wakati umeme ulikuwa unakatika na kurudi tulikuwa tunakoboa tani tatu kwa siku, lakini sasa tunakoboa tani 22 na tunafanya kazi muda wote."
Msimamizi wa udhibiti wa mifumo wa Tanesco, William Mkunya akitoa maelezo kuhusu uendeshaji wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara, Wilaya ya Kilomnero Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Good Samaritan, msimamizi wa hospitali hiyo, Father Charles Massawe amesema kituo hicho kimesaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kwani awali walilazimika kutumia jenereta ambalo walinunua dizeli ya Sh500,000 kwa mwezi.
"Changamoto iliyokuwepo hata umeme ukiwepo ulikuwa mdogo, hauwezi kuwasha baadhi ya mashine, lakini sasa hata kama umeme hautakuwepo tunapewa taarifa," amesema Father Massawe.