Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi Mbeya walia ubovu wa barabara kwenda makaburini

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Nonde jijini Mbeya akipita pembezoni mwa miundombinu barabara ya kutoka makaburini kuelekea Makyela jijini hapa. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Changamoto ya ubovu wa barabara inasababisha wananchi kubeba maiti za wapendwa wao mikononi umbali wa takriban kilometa moja hadi mbili kwa kuwa magari yanakwama hususan kipindi hiki cha mvua.

Mbeya. Wananchi wa Mtaa wa Nonde, jijini Mbeya wameiomba Serikali kuboresha barabara kutoka Makyela kwenda makaburini ili kuwapunguzia adha ya kubeba maiti mikononi umbali mrefu wanapokwenda kuzika.

Pia, wamemuomba mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kufikisha kilio hicho kwenye sekta husika, ili kuharakisha kuboreshwa kwa barabara hiyo muhimu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili Januari 28, 2024, wananchi hao wamesema barabara hiyo ni mbovu kwa miaka mingi, licha ya wakazi wa eneo hilo kuichonga mara kwa mara.

“Hii barabara ni kiungo muhimu, licha ya kuelekea kwenye makaburi, pia kuna mradi wa zahanati ya kijiji na Shule ya Msingi Nonde, hivyo kuna kila sababu Serikali kuitazama kwa jicho la kipekee,” amesema Abraham Joseph.

Amesema Serikali inapotekeleza miradi ya maendeleo iweke kipaumbele kwenye miundombinu ya barabara rafiki ambayo itasaidia jamii kuifikia na si kujenga kwa kuwakomoa watumiaji.

“Barabara hii ni mbovu kwa miaka nenda rudi, haijawahi kufanyiwa marekebisho, hata mbunge wetu, Dk Tulia Ackson ameshawahi kuishuhudia, mara kadhaa alishiriki misiba. Tunamuomba abebe kilio chetu kuwasilisha serikalini,” amesema.

Miongoni wa sehemu ya korofi ya barabara inayoelekea makaburi ya Nonde Jijini Mbeya ambayo inalalamikiwa na wananchi. Picha na Hawa Mathias

Mwanamke anayeishi katika mtaa huo, Mbushi Shitindi amesema kuna wakati magari yanayosafirisha mitihani yanakwama, hali inayowalazimu wasimamizi na walimu kubeba mikononi na kutembea umbali mrefu mpaka ilipo Shule ya Msingi Nonde.

“Hapo mitihani ikiibiwa, Serikali itahaha kuwakamata walimu kudai wamevujishwa bila kujali changamoto wanayokutana nayo wakati wa usafirishaji, ufike wakati kodi za wananchi zitumike kufika maeneo yasiyofikika ili kupunguza malalamiko,” amesema.

Diwani wa Nonde, Essay Nickson amesema mbali na changamoto hiyo ya barabara, pia kuna uchakavu wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi katika Shule ya Msingi Nonde.

“Kuhusu uchakavu miundombinu ya elimu nimefuatilia Jiji bila mafanikio, licha ya mambo mengine kufanya vizuri katika kata yangu. Naomba Serikali iliangalie suala hilo kwa upana wake,” amesema.

Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya elimu, Ofisa Elimu Msingi, Julius Lwinga amesema Serikali imetenga Sh3.8 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa matundu 16 ya vyoo katika Shule ya Msingi Nonde.

Akifafanua kuhusu ombi la ujenzi wa barabara ya Makyela kwenda makaburini, Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema kwa sasa itakuwa ngumu kutokana na ujenzi holela wa makazi kwenye hifadhi ya miundombinu hiyo.

“Endapo Tarura (Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini) wakisema waanze ujenzi kuna makazi lazima yataathirika kutokana na kusogea kwenye hifadhi ya barabara, nami nimewahi kupita niliposhiriki baadhi ya misiba, natambua changamoto yake,” amesema.

Amesema atawasiliana na Tarura kuona njia gani wataitumia ili kuboresha ikiwepo wananchi kupokea ushauri pale utakapohitajika, ili kuboresha na maiti zipitishwe katika barabara zilizo salama.