Wananchi kupewa elimu kuhusu El Nino

El Nino Morogoro. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amewataka wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kutoa elimu na tahadhari ya mvua za El Nino zikizotabiliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo.
Nderiananga ametoa wito huo jana mkoani hapa wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kilicholenga kutoa uelewa kwa kamati ya maafa ya mkoa na wataalamu wa namna ya kukabiliana na hali mafuriko, uharibufu na magonjwa ya mlipuko yatakayotkana na mvua hizo za El Nino ambazo zimetabiliwa kuanza mapema mwezi Oktoba mwaka huu.
Amesema kuwa katika utabili huo umeonesha mikoa 14 inayopata mvua misimu miwili ukiwemo Mkoa wa Morogoro itakumbwa na El Ninohivyo ofisi ya Waziri kitengo cha maafa imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na mvua hizo ambazo zimetabiliwa kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba 2023 hadi Januari 2024.
"Hatua hizo ni pamoja na waziri mkuu kutoa tamko la tahadhari ya kuwepo kwa mvua hizo na maagizo kwa mikoa yote ya namna ya kukabiliana na hali yoyote itakayotokea kutokana na mvua hizo lakini pia kutoa uelewa kwa kamati za maafa za mikoa na wataalamu," amesema Ngeriananga.
Aidha amezitaka kamati ya maafa za mkoa na wilaya kuandaa bajeti na vifaa kwa ajili ya kukabiliana na hali ya hatari itakayotokana na mvua hizo zinazotabiliwa kuwa juu ya wastani.
"Katika kufikisha elimu na tahadhari ya mvua hizi kwa wananchi lazima mtumie busara, sio leo hii hii mkawaondoe watu kwenye maeneo yao kwa kuwaambia eti Naibu Waziri kasema tuwaondoe, hapana nendeni mkawape elimu na tahadhari ya kukabiliana na chochote, yanapotokea mafuriko kunakuwepo na magonjwa ya mlipuko pia, miundombinu ya barabara inaharibika," amesema Ngeriananga.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba ameishukuru ofisi ya Waziri Mkuu Kamati ya Maafa kwa kuandaa elimu hiyo ambayo itatupa utayari wa kukabiliana na mvua hizo.
"Tunashukuru kwa kupewa elimu ya utayari na namna ya kukabiliana na kitakachotokea, Mkoa wa Morogoro ni mkoa uliotajwa kuwa katika hatari ya kupata mvua za Elnino hivyo elimu hii itatusaidia kujiandaa kwa kutoa tahadhari Kwa wanananchi wetu," amesema Waryuba.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa amewataka wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari mapema ikiwa ni pamoja na kusafisha mitaro na mifereji Ili kuruhusu maji ya mvua kupita.
Ameyataja maeneo hayo hatarishi kiwanni pamoja na Kihonda kwa bwana jela, Manyuki, Lukobe, Mafisa, Kichangani, Mwembesongo, Mkundi na Kwa upande wa Wilaya ya Morogoro ni pamoja na Mvuha, Kisaki na Ngerengere.
Wakati kamati za maafa zikijipanga na uwepo wa mvua hizo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limeanza linaendelea na mazoezi ya uokozi ikiwa ni moja ya maandalizi endapo yatatokea mafuriko.
Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Morogoro, Goodluck Zerote amesema aliwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa Kwa watoto ambao wamekuwa wakicheza kwenye mito, mabwawa hasa nyakati za mvua na kusababisha watoto hao kuzama na kusababisha madhara ikiwemo vifo.
"Katika kipindi hicho cha mvua mito itajaa nawasihi wananchi wasivuke kwenye mito wala makorongo yaliyojaa maji kwa kutumia vyombo vya moto Wala Kwa miguu kwani wanaweza kusombwa na maji na pale inapotokea hali ya hatari inayohitaji uokozi nawaomba wananchi watumie simu ya dharua ambayo ni bure 114 Ili waweze kupata msaada wa haraka," amesema Kamanda Zerote.
Mikoa iliyotabiliwa kupata mvua za Elnino kuwa ni pamoja na Geita, Kagera, Morogoro, Simiyu, Shinyanga, Pwani, Dar, Manyara, Mara, Kigoma, Tanga, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro.