TMA yatahadharisha mvua za El-Nino nchini

Muktasari:
- Yaelezwa kuwa mvua za El-Nino zitasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema matukio ya vifo, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu, yatashuhudiwa kuanzia Oktoba hadi Desemba 2023, kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha zikichangiwa na El-Nino.
Imeelezwa kuwa, mvua hizo zitasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira.
Kutokana na hali hiyo, TMA imezishauri sekta na taasisi mbalimbali, zikiwamo za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, wanyamapori, uchukuzi, mamlaka za miji, nishati, maji na madini, sekta binafsi, Wizara ya Afya na Menejimenti za Maafa kuchukua hatua mapema kabla ya kuanza kwa mvua hizo.
Mwelekeo wa kuanza kwa mvua hizo za vuli Oktoba hadi Desemba mwaka huu ulitangazwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a, akisema zinachochewa na uwepo wa El-Nino.
Alisema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu katika maeneo mengi nchini na zitakuwa za wastani na wastani wa juu itanyesha pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria.
Maeneo mengine ni magharibi inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo), ukanda wa pwani ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Kwa ukanda wa pwani kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili Oktoba, 2023 na kuisha wiki ya kwanza na ya pili ya Januari, 2024,” alisema Dk Chang’a.
Pia, alisema katika nyanda za juu kaskazini mashariki katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya Oktoba mwaka huu na kuisha wiki ya kwanza na ya pili ya Januari, 2024.
Wadau walivyojipanga
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana kuhusu taarifa hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe alisema watahakikisha elimu ya kujikinga na kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko inaendelea kutolewa kwa wananchi.
“Hatua zipo wakati wote tunachukua, hasa kudhibiti mazalia ya mbu, kuwaelewesha watu kutumia maji safi kuepuka magonjwa ya mlipuko, kwa hiyo, hatua tunazochukua ndizo zile zile tunazochukua wakati wote kwa lengo la kuhakikisha tunawapa elimu ya afya wananchi,” alisema Dk Shekalaghe.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), Victor Seff alisema asilimia 71.48 ya mtandao wa barabara za wilaya ni za udongo, hivyo wameweka mkakati wa kuzifanyia marekebisho mapema.
“Barabara hizi huathirika wakati wa mvua na kusababisha maeneo mengi kutopitika, hivyo kudhoofisha ukuaji wa sekta ya kilimo,” alisema Seff.
Alisema changamoto hiyo pia husababisha kupandisha gharama za usafiri na usafirishaji na kutofikika kwa huduma za kijamii na kiuchumi kwa maeneo mengi ya pembezoni.
Ili kukabiliana na hilo, Seff alisema wana mpango wa muda mfupi wa kila mwaka na ule wa kati wa miaka mitano unaoendana na mipango ya kitaifa na kimataifa ya muda mrefu.
Hata hivyo, Dk Kang’a wa TMA alisema kwa kushirikiana na wataalamu wa sekta zote zitakazoathiriwa na mvua hizo, wametoa mbinu za kuzikabili athari zitakazojitokeza.
“Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama kwenye mashamba yao, mmomonyoko na upotevu wa rutuba sambamba na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa vuli,” alisema Dk Kang’a.
Akizungumzia mamlaka za miji na wilaya, Dk Kang’a alisema mvua kubwa husababisha kutuama kwa maji na mafuriko.
Alisema hali hiyo husababisha uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali. “Mamlaka za miji zinashauriwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mafuriko sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa,” alisema Dk Kang’a.
Alizitaja hatua hizo ni kuimarisha kamati za maafa ngazi za kijiji na wilaya ili waweze kujiandaa na kupunguza athari pindi zitakapotokea.
Dk Kang’a alisema maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani yanaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira.
“Hivyo, Idara ya Menejimenti ya Maafa nchini inashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Dk Kang’a.
Pia, alisema magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mazingira.