TMA yatoa angalizo hali mbaya ya hewa siku tano mfululizo

Muktasari:
- Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la hali mbaya ya hewa inayotarajia kutokea kwa siku tano mfululizo katika maeneo ya maziwa makuu na bahari.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la hali mbaya ya hewa inayotarajia kutokea kwa siku tano mfululizo katika maeneo ya maziwa makuu na bahari.
Katika taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo Jumatatu Agosti 7, 2023 imetoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita 2 kuanzia leo hadi Ijumaa Agosti 11, 2023.
Maeneo ambayo yametajwa kuathirika ni maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi (Mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na Pwani) ikijumuisha visiwa vya Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha, imesema baadhi ya athari zinaweza kujitokeza kutokana na hali hiyo zikiwemo kuathirika kwa shughuli za uvuvi na usafirishaji.
Hali hii inatarajiwa kutokea katika maeneo hayo kwa siku hizo tano huku kiwango cha kutokea kwa hali hiyo na athari zake kikitajwa kuwa ni wastani.
TMA imewataka wananchi waishio katika maeneo yaliyotajwa kujiandaa na mabadiliko hayo ya hali ya hewa na kuchukua tahadhari.