Wananchi Kigoma waomba ukarabati meli tatu uwahishwe

Muktasari:
Wakazi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma wameomba kukamilishwa kwa wakati ukarabati wa Meli ya Mv Liemba, Mv Mwongozo na Mt Sangara inayobeba mafuta kutoka Tanzania kwenda nchi za jirani ili kurahisisha shughuli zao za usafirishaji mizigo.
Kigoma. Wakazi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma wameomba kukamilishwa kwa wakati ukarabati wa Meli ya Mv Liemba, Mv Mwongozo na Mt Sangara inayobeba mafuta kutoka Tanzania kwenda nchi za jirani ili kurahisisha shughuli zao za usafirishaji mizigo.
Wakizungumza Novemba 27, 2023 wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wamesema wanalazimika kutumia maboti kwaajili ya kusafiri na kutuma mizigo yao jambo ambalo linawafanya kutokuwa huru na kuhofia usalama wao.
Mkazi wa mjini Kigoma, Salum Hassan amesema kusimama kwa shughuli za meli hizo kumewakwamisha katika biashara zao ikilinganishwa na awali walipokuwa wakizitumia akidai kuna umuhimu mkubwa wa kuharakisha marekebisho ya meli hizo.
Naye Shamsa Saimon amesema usafiri wao mkubwa ni meli ambazo wamekuwa wakizitumia kwenda nchi jirani kwenye shughuli zao za kibiashara hivyo kutokamilika kwa wakati kunachangia kushusha uchumi wao na uchumi wa mkoa huo.
Kaimu Meneja wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Mkoa wa Kigoma, Allen Butembero amesema ukarabati wa MT Sangara umefikia asilimia 92 ambayo inabeba tani 350 sawa na lita 410,000 na inatarajia kukamilika Aprili,2024 kwa gharama za Sh8.4 bilioni.
“Meli ya MT Sangara inabeba mafuta ya petrol, dieseli na mafuta ya taa, inafanya safari zake kutoka Kigoma kwenda bandari ya Kalemii,Uvira nchi ya Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi,”amesema Butembero
Butembero amesema ukarabati wa meli ya Mv Liemba inayobeba abiria 600 na tani 200 za mizigo itachukua mwaka mmoja na nusu kukamilika akidai ukarabati wake utaanza Januari, 2024 kwakuwa mkandarasi yupo katika hatua za awali za kuleta vifaa kwaajili ya kuanza ukarabati utakao gharimu Sh32 Bilioni.
Naibu Waziri wa uchukuzi, David Kihenzile amesema kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati kutasaidia wananchi kuwa na fursa za kusafirisha bidhaa zao katika nchi za maziwa makuu na kuchochea uchumi wa ukanda huo.
“Niagize wakandarasi wote wa Mkoa wa Kigoma wazingatie ubora wa miradi yao kwenye sekta ya uchukuzi, wazingatie muda wa utekelezaji wa miradi yao na wahakikishe wanatumia vibarua wa eneo husika na kuwalipa posho zao kwa wakati,”amesema Kihenzile