Wananchi 500 kunufaika na elimu ya uwekezaji nchini

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (wa kwanza kushoto) akiwa katika banda la kituo cha uwekezaji nchini (TIC) wakati wa ziara yake kwenye maonyesho ya kimataifa ya Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, katikati ni mwekezaji wa Kampuni ya Levy Africa Ltd, Christopher Mwasambili na kulia ni Kaimu Meneja wa TIC, Nyanda za Juu kusini, Deusidedit Hokororo.
Muktasari:
- Maoneosho ya Nane nane yanafanyika kwa mara ya kwanza kimataifa jijini hapa lakini ikiwa ni ya tisa kufanyika mkoani Mbeya kitaifa na mwaka huu yatafikia tamati Agosti 8 huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mbeya. Kituo cha uwekezaji nyanda za juu Kusini (TIC) kimesema kimejipanga kitoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi zaidi ya 500 katika maonesho ya kimataifa Nanenane huku kikitangaza kupunguza gharama za thamani ya mradi kwa wawekezaji wa ndani kutoka dola 100,000 hadi 50,000.
Akizungumza kwenye maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini hapa leo Agosti 5, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exhaud Kigahe, Kaimu meneja wa kituo hicho kanda hiyo, Deusidedit Hokororo amesema watatumia maonesho hayo kuwapa elimu wawekezaji wa ndani.
Amesema katika kutambua umuhimu wa wawekezaji hao, kituo cha TIC kimepunguza gharama ya thamani ya mradi kutoka dola 100,000 hadi dola 50,000 ikiwa ni sheria mpya ya mwaka 2022.
"Hizi ni juhudi na mipango kazi ya kituo cha uwekezaji nchini (TIC) katika kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani, lakini tumejipanga kutumia maonesho haya kutoa elimu kwa zaidi ya wananchi 500 ndani na nje ya kanda ya hii"
"Hii sheria inaenda kuwasaidia wawekezaji wa ndani ambapo kama wataongeza muda na kupata cheti cha usajili kutoka TIC watapata nafuu ya faida za kikodi na zisizo za kikodi ikiwamo huduma mbalimbali," amesema Hokororo.
Kwa upande wake Naibu waziri Kigahe amesema hatua hiyo ni nzuri na inaweza kuleta matokeo chanya akimuomba muwekezaji wa kampuni ha Levy Africa Ltd ambao ni wawekezaji katika mnyololo wa wa zao la Kokoa kwa kuongeza thamani Christopher Mwasambili kukamilisha taratibu zote ili kufuangua rasmi kiwanda ambacho kitajengwa wilayani Kyela mkoani hapa.
"Kupitia stakabadhi ya ghala imepanda kutoka Sh 4,000 hadi Sh 7,500 sasa tatizo liko wapi, kamilisha taratibu ufungue hicho kiwanda kikubwa, labda kama hujapata soko au bidhaa za kutosha" amesema Kigahe.
Naye muwekezaji huyo, Mwasambili amesema hadi sasa kampuni hiyo ipo hatua za mwisho na kwamba watakuwa wakitoa tani 600 na kwamba zipo aina 24 ambazo zitatumika.
"Hiki ni kiwanda kikubwa ambapo shughuli zake zitaanza hivi karibuni na tutatoa hadi tani 600, shirika la viwango nchini (TBS) tayari tumemalizana nao hivyo ni hatua ndogo zimebaki tukamilishe na kazi kuanza," amesema Mwasambili.
Mmoja ya wajasiriamali waliopo katkka maonesho hayo, Halima Pesambili ameshauri uwekezaji wowote kuanza na wazawa inapotokea fursa za ajira zikiwamo za moja kwa moja na zile za muda ili kumpa thamani mtanzania.
"Nafikiri hawa wawekezaji wawe wa ndani au nje kiwepo kipengele maalumu cha kuanza na wazawa pale inapotokea fursa za ajira, hii italeta thamani na heshima kwa nchi yetu," amesema Halima anayejishughulisha na utengenezaji wa nguo za batiki.