Wananchi 10,000 Arusha kupatiwa matibabu bure


Muktasari:

Wananchi 10,000 katika mkoa wa Arusha kesho watafanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa siku tano na kupatiwa dawa na miwani bure. Wananchi 10,000 katika mkoa wa Arusha kesho watafanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa siku tano na kupatiwa dawa na miwani bure.

Dar es Salaam. Jopo la madaktari bingwa 24 wanatarajiwa kuendesha kambi ya matibabu kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambapo zaidi ya wakazi 10,000 watapatiwa huduma za uchunguzi bure.

  

Kambi hiyo, itaanza Desemba 5 hadi 9, 2022 ikiambatana na huduma za uchunguzi kwa magonjwa ya ndani, utoaji dawa na miwani bure kwa wagonjwa.


Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, leo Jumapili Desemba 4, 2022, Mganga Mfawithi wa Hospitali hiyo Dk Alex Ernest amesema katika kambi hiyo wanataraji kuhudumia wananchi 2,000 wenye matatizo mbalimbali kwa siku moja.


“Kesho (Jumatatu) tutaanza kambi maalumu asubuhi hapa hospitalini, tutatoa huduma ya ushauri wa magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, figo, matatizo ya njia ya mkojo, macho, masikio, koo na pua, matatizo ya ngozi na usikivu na meno.


Pia, tutashughulika na wagonjwa waliopata majeraha yatokanayo na ajali pamoja na upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za uchunguzi na dawa ni bure kwa wale wenye bima ya afya ni muhimu waje nazo,” amesema.

Dk Ernest amesema vipimo vya magonjwa mbalimbali vitalipiwa lakini uchunguzi wa vipimo vya awali utatolewa bure.

Kwa upande wake, Saitoti Laizer, mkazi wa mkoa huo amesema, kambi hiyo itawapa fursa kufahamu afya zao,

“Bila hamasa si rahisi mtu kwenda kupima wakati haumwi, jambo linalofanyika ni jema mtu anaweza kutoka kazini akapita kupima ugonjwa wowote na akapewa dawa bure, kwa kweli hatuna utaratibu wa kupima hadi tuumwe, kwahiyo Serikali imefanya vyema kuja na mpango huo,” amesema.

Ni kwa mara ya pili Hospitali ya Mount Meru inaendesha kambi hiyo ambapo mwaka jana, madaktari bingwa 17 walitoa huduma kwa watu zaidi ya 9,800 wa mkoa huo  ikiwa ni sehemu ya kusherekea miaka 60 ya Uhuru.