Wanafunzi watua kero za shule yao kwa mbunge
Wanafunzi wa shule ya msingi Nanjoka, wakifurahia jambo baada ya mbunge wa jimbo hilo kuwatembelea shuleni hapo
Muktasari:
- Wanafunzi wa shule hiyo wamebainisha changamoto hizo leo Februari 23, 2026 wakati wa ziara ya mbunge wa Jimbo la Tunduru (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, aliyetembelea shule hiyo aliyosoma ili kujua changamoto zake.
Tunduru. Shule ya Msingi Nanjoka iliyopo Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, inakabiliwa na changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, vitabu vya kujisomea pamoja na vifaa vya michezo.
Wanafunzi wa shule hiyo wamebainisha changamoto hizo leo Februari 23, 2026 wakati wa ziara ya mbunge wa Jimbo la Tunduru (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, aliyetembelea shule hiyo aliyosoma ili kujua changamoto zake.
Mwanafunzi Venance Makelle amemuomba mbunge huyo kuwasaidia kuwajengea matundu ya vyoo pamoja na kuwaletea vifaa vya michezo, kwani wanashindwa kucheza kutokana na kukosekana kwa vifaa hivyo.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Nanjoka, wakati alipokwenda kuwatembelea kusikiliza changamoto zao.
“Tunakuomba mbunge utusaidie kutupatia vifaa vya michezo, tunashindwa kucheza kutokana na kukosekana kwa vifaa. Pia, tunaomba utuongezee matundu ya vyoo kwani yaliyopo sasa hayatoshi,” amesema Makelle.
Naye Munira Said, mwanafunzi wa darasa la sita, amemuomba mbunge huyo kuwasaidia kuwapatia vitabu kwani shule yao inakabiliwa na changamoto ya vitabu vya kujisomea.
“Tunashindwa kujisomea kwa kuwa shule haina vitabu vya kutosha, tunakuomba mbunge utusaidie kupata vitabu ili tujisomee vizuri,” amesema Munira.
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Nanjoka, Hussein Mkwiya amemuomba mbunge kuwasaidia kuongeza madarasa pamoja na madawati katika shule hiyo, kwani kuna baadhi ya madarasa wanafunzi wanakaa chini na wengine wanapishana muda.
Wanafunzi wa shule ya msingi Nanjoka, wakifurahia jambo baada ya mbunge wa jimbo hilo kuwatembelea shuleni hapo
“Tunaomba utusaidie kuongeza madarasa pamoja na madawati kwani kuna baadhi ya madarasa wanakaa chini na wengine kupishana muda kutokana na upungufu wa uliopo,” amesema.
Akijibu changamoto hizo, Shaibu amemtaka diwani huyo kuandika barua kwa halmashauri na kuomba fedha za mfuko wa jimbo ili waweze kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza madawati pamoja na kununua saruji kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa madarasa.
“Diwani, andika barua halmashauri kuomba fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya madawati pamoja na saruji ili tuanze kwa ujenzi wa madarasa sisi wenyewe,” amesema Shaibu.
Mbunge huyo anaendelea na ziara hiyo yenye lengo la kutoa mrejesho wa Bunge lililopita na kukusanya maoni kuelekea Bunge lijalo la bajeti.