Wanafunzi, vijana 252 wenye ualbino waweka kambi Mwanza

Baadhi ya vijana wenye ualbino wakifrahia kwenye Summer camp jijini Mwanza. Picha Saada Amir
Muktasari:
Kambi ya wanafunzi hao wanaofadhiliwa na Shirika la Under the Same Sun (UTSS) imeanza jana Agost 5 na kutarajiwa kufungwa Agost 12, 2023 itakayohusisha upimaji wa afya, kliniki ya ngozi, kliniki ya macho na kliniki ya masikio kwa watu hao wenye ualbino.
Mwanza. Zaidi ya wanafunzi na waajiriwa 252 wenye ualbino kutoka mikoa mbalimbali nchini wamekutana jijini Mwanza kwenye kambi ya majira ya joto (Summer Camp) kwaajili ya kupeana faraja, kubadilishana mawazo, kushauriana na kufrahi kwa pamoja .
Kambi ya wanafunzi hao wanaofadhiliwa na Shirika la Under the Same Sun (UTSS) imeanza jana Agost 5 na kutarajiwa kufungwa Agost 12, 2023 itakayohusisha upimaji wa afya, kliniki ya ngozi, kliniki ya macho na kliniki ya masikio kwa watu hao wenye ualbino.
Mratibu wa camp hiyo, Grace Wabanhu amesema imegawanyika sehemu mbili ambayo ni wanafunzi wa shule ya msingi hadi kidato cha nne na nyingine inayojumuisha kuanzia kidato cha tano, vyuo vikuu na walioajiriwa.
“Hii ni camp yetu ya nne kufanya na huwa tunafanya kila baada ya miaka miwili ambayo inawaonganisha wanafunzi wenye ualbino wanaofadhiliwa na UTSS, wanafunzi hawa ni kutoka shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu,”
“Lengo ni kuwakutanisha vijana hawa wenye ualbino pamoja kwa sababu wanafadhiliwa na shirika moja na wanasoma sehemu tofauti tofauti kwahiyo wakikutana kwanza ni faraja, kubadilishana mawazo, kushauriana lakini pili ni kufrahi kwa pamoja sababu vijana hawa wamepitia mengi,”amesema Grace
Amesema vijana hao wengi wao waliochukuliwa na UTSS wakiwa wadogo wengi wao wamefika vyuo vikuu wakitokea kwenye mazingira ambayo yalikuwa ni duni na wengine walikutana na madhira kipindi ambacho kulitokea mauaji ya wenye ualbino.
“Walikuwa na simanzi lakini kwa sasa tunaanza kuona wanafrahia wengine wamefika vyuo vikuu na wengine tayari wamesha ajiriwa ambao watawasihi wenzao katika masomo na mambo mengine,
“Sasa katika camp hii tutafanya kliniki ya ngozi kama tunavojua watu wenye ualbino tuna athiriwa na mionzi ya jua kwahiyo mara kwa mara nilazima tufanye kliniki ya ngozi, tutafanya kliniki ya macho kwa sababu tuna uoni hafifu hivyo tutajua nani anahitaji miwani na nani ana changamoto ya macho lakini pia tutafanya kliniki ya masikio kwa sababu tumekuwa tukipata changamoto kwa wanafunzi baadhi ambao wanapoteza hali ya kusikia lakini pia jinsi ya kutunza masikio yao,”amesema
Katika kambi hiyo, wanafunzi na vijana hao wenye ualbino watajifunza neno la Mungu, watakuwa na darasa la kujua vipaji vyao na fani wanazopendelea, watakuwa na darasa la maarifa ya jamii kuweza kujua wanaishije na jamii, darasa la sanaa, darasa la muziki pamoja na michezo mbalimbali.
Mmoja wa wanafunzi aliyehudhuria camp hiyo, Salim Rashid amesema kupitia jumuiko hilo watajifunza masuala mbalimbali na kupata uzoefu kutoka kwa wenzao.
“Tunamshukuru muanzilishi wa UTSS, Peter Ash kwa kutuwezesha kutimiza ndoto zetu kupitia ufadhiri wa masomo na kutufanya vijana tunaojiamini, kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii na wenye furaha,”amesema Rashid