Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

LHRC walaani mauaji ya mwenye ualbino Mwanza

Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,kuhusu kituo hicho kulaani tukio la mauaji ya mtu mwenye ualbino,Joseph Mathias mkazi wa Mwanza Wilayani Kwimba Kata ya Ngula, kulia ni Mwenyekiti TAS Taifa, Mussa Kabimba. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Tukio hilo la mauaji lililotokea Novemba 2, 2022 katika kata ya Ngula iliyopo wilayani Kwimba, mkoani Mwanza ambapo mwanaume huyo aliuawa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani Kwake amelala.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) wamelaani mauaji ya mtu mwenye ualbino, Joseph Mathias kwa kile kinachotajwa kuwa ni Imani za kishirikina.

Tukio lililotokea Novemba 2, 2022 katika kata ya Ngula iliyopo wilayani Kwimba, mkoani Mwanza ambapo mwanaume huyo aliuawa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani Kwake amelala.

Mathias mwenye umri wa miaka 50 alikatwa mkono wa kulia, hali ambayo ilimsababishia kutokwa na damu nyingi hadi kufikwa na umauti.

Akizungumzia tukio hilo leo Novemba 7, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema wanaunga mkono juhudi ambazo zimeanza kufanywa na mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa siku saba kwa jeshi la polisi mkoani humo kuhakikisha wanawakamata watu waliohusika katika mauaji hayo.

“Tunatoa wito wakishawakamata watu hao, mrejesho utolewe wazi wazi ili kuondoa taharuki na hali ya woga kwa kundi hili la watu wenye ualbino,” amesema Henga.

Henga ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 hakukuwa na ripoti yoyote ya mauaji dhidi ya watu wenye ualibino anasema hiyo yote ni baada ya juhudi za jeshi la polis Tanzania, asasi za kiraia, Mahakama na Tume ya Haki za Binadamu nchini kuhakikisha vitendo hivyo havitokei.

“Kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, vitendo mbalimbali vya mauji ya albino yameendelea kutokea, jambo ambalo linatishia amani kwa watu hao wenye ulemavu,” amesema mkurugenzi huyo.

Pia, amesema ni wazi kuwa soko haramu la viungo vya watu wenye ualbino (black market) linalohisiwa kuratibiwa na waganga wa kienyeji bado lipo kutokana na uendelevu wa imank za kishirikiana katika jamii.

Nae Katibu Mkuu TAS, Mussa Kabimba amesema jitihada nyingi zinafanywa na wadau kama asasi za kirai lakini kwa upande wa serikali bado hawana mkakati thabiti kwani wao huwa wana mipango ya dharura lakini mipango ya muda mrefu bado hawana.

“Bado kuna utashi hafifu kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watu wenye ualbino,” amesema Kabimba.

Kadhalika, LHRC na TAS wametoa wito kwa serikali na jeshi la polisi kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa, upelelezi unafanyika kwa wakati na wanafikishwa mahakamani.