Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi shule kongwe ya Kibohehe warejea masomoni

Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Amiri Mkalipa mwenye shati ya kaki kushoto na balozi wa Japan nchini, Yosushi Misawa mwenye shuka la bluu wakiweka jiwe la msingi katika makabidhiano ya Shule ya Msingi Kibohehe iliyojengwa na Serikali ya Japan katika kijiji cha Roondoo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Unaweza kusema ni neema iliwashukia baada ya majonzi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Kibohehe iliyopo Kijiji cha Rondoi baada ya kupata majengo mapya ya shule baada ya yale yaliyokuwa chakavu kudondoka na kusababisha kifo cha mwanafunzi.

Moshi. Zaidi ya Sh206 milioni zilizotolewa na Serikali ya Japan zimesaidia kurejesha tabasamu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibohehe iliyopo Kijiji cha Roondoo, Wilaya ya Hai baada ya shuke yao kujengwa upya baada ya darasa kudondoka na kusababisha kifo cha mwanafunzi.

Darasa hilo lilidondoka kufuatia upepo na mvua iliyokuwa ikinyesha Februari 2020 wakati wanafunzi wakiendelea na masomo. Mbali na kifo pia wanafunzi wanne walijeruhiwa katika tukio hilo.

Flora Natai ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Kibohehe amesema kufuatilia shule hiyo kudondoka na kusababisha madhara, Serikali iliamua kuifunga na wanafunzi waliokuwapo walihamishiwa shule za jirani na makazi yao.

Natai ameyasema hayo wakati Japan ikikabidhi shule hiyo kwa Serikali ya Tanzania ikiwa ni baada ya ujenzi kukamilika na wanafunzi kurejea.

Natai amesema kudondoka kwa ukuta huo kulichangiwa na uchakavu wake kwani ilijengwa tangu mwaka 1947.

"Wakati inadondoka kutokana na upepo mkali na kusababisha madhara kwa wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo, mwanafunzi mmoja alifariki dunia na wanne kujeruhiwa jambo lililoifanya serikali iifunge shule hiyo," amesema Natai huku akishindwa kuzuia machozi yake.

Amesema baada ya shule kufungwa na wanafunzi kuhamishiwa shule tofauti kulingana na umbali wa maeneo yao, wanakijiji walilazimika kuanza kujichangisha fedha ili kusaidia watoto wao ambapo walifanikiwa kupata Sh6 milioni.

Pia wadau mbalimbali wa maendeleo na Serikali zilichangia Sh17. 45 milioni ambazo zilifanya ujenzi kuanza kabla ya wao kupata fedha kutoka Serikali ya Japan.

"Tulipokamilisha ujenzi kuna kiasi cha fedha kilibakia hivyo tukaomba ruhusa kutoka Japan na tukaweza kutumia fedha hizo kutengeneza madawati 184, meza 5 na viti vitano kwa ajili ya walimu," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wengine 206, Muksin Kimaro amesema ni furaha kwao kujifunza katika mazingira mapya tofauti na zamani walipokuwa na wasiwasi.

"Madarasa yalikuwa chakavu, hatuko huru, sasa tunasoma vizuri, madarasa mazuri, mapya," amesema Kimaro ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita.

Balozi wa Japan nchini, Yosushi Misawa amesema madarasa hayo yamejengwa kupitia mpango wa Misaada uitwayo “Grant Assistance for Grassroots Human Security Projects (GGHSP) ulioanza mwaka wa 1989 ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi zinazoendelea.

Amesema mpango huo unalenga kufikia ulimwengu ambao hakuna mtu anayeachwa nyuma bali watu wote wanaweza kuishi kwa amani na kushikana mikono pamoja na kila mtu katika kila kona ya dunia.

Amesema anaamini mpango huu una maana kubwa sio tu kwa watu wanaofaidika moja kwa moja kupitia misaada hiyo, lakini pia kwa watumishi wa ubalozi, na Serikali ya Japan.

"Kupitia upangaji na utekelezaji wa GGHSP, tunapata fursa muhimu ya kuwasiliana moja kwa moja na wananchi wa kawaida wa Tanzania walioko vijijini,  kujifunza matatizo na changamoto ambazo watu wanakumbana nazo katika maisha yao ya kila siku wanapofanya kazi, kulea watoto wao na kuishi," amesema Misawa.

Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo, amesema wafanyakazi wa Japan waliokuwa eneo hilo walipogundua walipendekeza shule hiyo kujengwa upya badala ya kukarabati eneo lililoleta madhara pekee.

"Leo, nina furaha kuona jengo jipya la madarasa limekamilika kwa mafanikio na zaidi ya wanafunzi 200 wanafurahia kusoma hapo. Natumaini itatumika ipasavyo na kudumishwa ipasavyo kwa muda mrefu. Na itachangia maendeleo zaidi ya watoto na shule hii," amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Edmund Rutalaka amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh1 bilioni ili kuendeleza ukarabati wa shule kongwe zilizopo katika wilaya hiyo katika ngazi ya msingi na sekondari.

"Tunafahamu kuwa karibu asilimia 50 ya shule zilizopo wilayani Hai zinahitaji ukarabati, tumeanza kupitia fedha zilizotengwa na tutaendelea kufanya maboresho hayo," amesema Rutalaka.